NEWS

Monday, 14 July 2025

Manufaa lukuki ya ubia wa Barrick, Serikali kupitia Twiga yaonekana wazi kwa vitendo



Rais na CEO wa Barrick, Mark Bristow (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari (hawapo pichani) kwenye ukumbi wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu wilayani Kahama, Shinyanga mwanzoni mwa wiki iliyopita.
---------------------------------------

Na Mwandishi Maalumu

Mafanikio ya ubia kati ya Kampuni ya Kimataifa ya Madini ya Barrick na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals siyo hadithi tena ya kusimuliwa, bali ni ukweli ulio dhihiri, ambao kila mwenye macho hambiwi tazama.

Miaka mitano ya ubia huu imeshuhudia mabilioni ya shilingi yakiingizwa kwenye uchumi wa taifa hili kubwa katika Afrika Mashariki ili kuboresha maendeleo mbalimbali katika sekta za kijamii kama vile elimu, afya, maji, nishati na barabara, kwa kutaja chache.

Kama alivyosema hivi karibuni, Rais na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Barrick, Mark Bristow, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu, “ubia huo umejenga mfano endelevu wa uendelezaji wa rasilimali madini nchini Tanzania.”

Kwa sasa, sekta ya madini nchini inachangia asilimia 10.1 kwenye Pato la Taifa, jambo ambalo kwa miaka ya nyuma ilikuwa hadithi ya kufikirika.

Tangu kuasisiwa kwa ubia huu mwaka 2019, sekta ya madini imevaa sura mpya katika maendeleo ya taifa kwa kuongezewa thamani, ubora wa uendeshaji na uwekezaji wa muda mrefu katika kujenga Tanzania mpya.

Lengo kubwa la kuanzishwa kwa ubia huu, kama Bristow anavyobainisha, lilikuwa kujenga mustakabali mpya kwa kuufungua utajiri wa dhahabu wa Tanzania kwa njia inayogawanya kwa haki manufaa yake na kujenga thamani ya kudumu kwa wadau wote.

Katika kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa kutimiza lengo hili, Barrick imekuwa mchangiaji mkubwa katika uchumi wa nchi kupitia sekta ya madini.

Trilioni 12/- zaingizwa
kwenye Uchumi nchini
Hadi leo tunapozungumzia mchango wa Barrick katika maendeleo ya Tanzania, tunazungumzia kuingizwa kwa shilingi zaidi ya trilioni 12 (Dola bilioni 4.79) katika uchumi wa taifa, ikiwa ni pamoja na Dola milioni 558 katika nusu ya kwanza ya mwaka huu.

Isitoshe, asilimia 90 ya ununuzi wa bidhaa na huduma unafanyika kutoka kampuni za Kitanzania, ambazo nyingi ni za wazawa wanaofaidika na uwepo wa Barrick.

Migodi yazalisha ajira
kwa Watanzania

Zaidi ya hayo, asilimia 95 ya wafanyakazi katika migodi ya Barrick hapa nchini, kwa mujibu wa Bristow, ni Watanzania ambao kati yao asilimia 49 wanatoka vijiji vilivyo jirani na migodi.

Katika dunia ambayo inakabiliwa na tatizo kubwa la ajira kwa vijana, kwa hakika migodi ya Barrick – Bulyanhulu na North Mara, imeleta ahueni kwa wananchi na kupunguza kuhangaika kwao, hasa kwa wale wanaoishi karibu na migodi hiyo.

Licha ya ajira, wananchi waishio jirani na migodi wamenufaika kwa kuanzisha huduma na shughuli mbalimbali za kiuchumi ambazo chimbuko lake kubwa ni kuwepo kwa migodi katika maeneo yao.

“Idadi ya kampuni za ndani zinazofanya biashara na migodi ya Barrick zimeongezeka maradufu. Hii inaonesha dhahiri jinsi uwepo wetu unavyowanufaisha Watanzania kutokana na matunda ya kuwepo kwa migodi,” anaeleza Bristow.

Naibu Waziri asema ubia
ni kielelezo cha ushindi

Serikali ya Tanzania inafurahishwa na uendeshaji na michango ya migodi ya Barrick katika uchumi wa taifa kwa sababu imeiweka nchi katika ramani ya dunia kwa kuwa taifa linalotambulika kwa rasilimali madini.

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Stephen Kiruswa, anasema ubia wa Barrick na Serikali ya Tanzania ni chanda na pete kwa sababu ni kielelezo cha mafanikio.

“Mradi huu wa ubia ni kielelezo cha dhana ya uwazi jinsi unavyoendeshwa. Barrick wameonesha kwa vitendo utekelezaji wa sheria ya maudhui ya ndani (local content) kwa kuwashirikisha Watanzania kunufaika na sekta ya madini,” anaeleza Dkt. Kiruswa.

Kauli ya Waziri Kiruswa inaungwa mkono na Rais wa Barrick kwamba pande zote zinazounda ubia kupitia kampuni ya Twiga zinanufaika na matunda ya migodi ya Bulyanhulu ulioko wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, na North Mara wa wilayani Tarime, mkoani Mara.

Kwa mtu yeyote anayetembelea vijiji vilivyo jirani na migodi hiyo ataona mageuzi yaliyopatikana katika nyanja mbalimbali za maendeleo – elimu, afya, maji, nishati na barabara.

Sura za vijiji karibu na migodi hiyo zimeshuhudia kasi ya mabadiliko ya kuwepo huduma muhimu za shule za kisasa, zahanati na vituo vya afya, upatikanaji wa maji safi na salama, barabara zinazopitika misimu yote na huduma ya umeme, ukiachilia mbali hali ya ustawi wa maisha ya wananchi wenyewe kiuchumi.

Katika Tanzania inayokimbia kwa kasi kuelekea uchumi wa kisasa, ubia wa Barrick na Serikali ni mfano wa kuigwa kwa sababu umechochea ukuaji wa sekta ya madini na kuifanya Barrick kuwa mlipaji mkubwa wa kodi kitaifa ikilinganishwa na taasisi nyingine.

Ndoto ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, imeanza kutimia. Miaka ya mwanzo wa uhuru, gwiji huyo wa siasa barani Afrika alipata kusema kwamba lazima taifa linufaike na rasilimali zake, yakiwemo madini.

Mwalimu aliamini katika usimamizi mzuri wa sekta ya madini ili iweze kuchochea maendeleo ya nchi. Aliamini kwamba sekta imara ya madini itachochea ukuaji wa Pato la Taifa kwa kufuata misingi ya kuendeleza rasilimali hiyo.

Dira hiyo ya Mwalimu Nyerere ndiyo inayofuatwa na Serikali ya Awamu ya Sita chiniya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha kwamba sekta ya madini inakuwa na mchango mkubwa kwa uchumi wa taifa. Kila kitu kinawezekana, jambo la msingi ni kutimiza wajibu.
Read Also Section Example

Unaweza pia kusoma:

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages