Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akizindua Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC), jijini Dodoma, Julai 17, 2025.
-------------------------------------------
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa Watanzania wote kushiriki katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ili kufikia lengo kuu la kujenga taifa jumuishi, lenye ustawi, la haki na linalojitegemea.
Rais Samia aliyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa Dira hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC), jijini Dodoma, jana Julai 17, 2025.
Rais Samia alisema Dira 2050 ni matokeo ya mchakato jumuishi uliohusisha maoni ya wananchi na wadau wote, na inalenga kufanikisha maendeleo jumuishi kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Aidha, alisema Dira hiyo iliyozingatia matarajio ya Watanzania, imejengwa juu ya msingi wa mafanikio na mafunzo ya historia ya maendeleo ya Tanzania tangu Uhuru, ikiwa ni pamoja na mafanikio na changamoto ya utekelezaji wa Dira ya 2025.
“Maudhui ya Dira 2050 yametokana na maoni na matakwa ya Watanzania wenyewe. Tumefikiri wenyewe, tumeandika wenyewe, tumepanga wenyewe na tutatekeleza wenyewe,” alisema Rais Samia.

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
akizungumza katika hafla hiyo.
---------------------------------------
Rais Samia alisema uandaaji wa Dira hiyo umezingatia muktadha wa sasa wa dunia unaogusa masuala muhimu kama vile mabadiliko ya mfumo wa uchumi wa dunia, mabadiliko ya tabianchi, ongezeko kubwa la vijana nchini na mapinduzi ya kiteknolojia.
Aliongeza kuwa kwa ukubwa wa rasilimali, ari na uwezo wa wananchi, Tanzania ina kila sababu ya kuweka na kufikia malengo makubwa ya maendeleo iliyojiwekea, ikiwa ni pamoja na lengo kuu la kuwa nchi ya kipato cha kati cha juu yenye uchumi wa Dola Trilioni Moja ifikapo mwaka 2050.

Rais Dkt. Samia akimkabidhi Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kitabu cha Dira 2050.
----------------------------------------
Rais Samia pia alisema ili kufikia utekelezaji wa Dira 2050, ipo haja ya kufanya mabadiliko ya kifikra, kimtazamo na kimatendo ili kufanikisha malengo yake, akiongeza kuwa utekelezaji wa Dira hiyo unahitaji ushirikiano wa Serikali Kuu, Mamlaka ya Serikali za Mitaa, sekta binafsi, jamii, taasisi za dini, mashirika ya kiraia na wananchi mmoja mmoja.
Katika hilo, Rais Samia aliielekeza Tume ya Taifa ya Mipango kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kuandaa mifumo madhubuti ya ufuatiliaji na tathmini pamoja na vigezo vya kupima utendaji wa kila taasisi ya umma kwa kila hatua ya utekelezaji.
Vilevile, aliziagiza wizara zote kufanya mapitio ya sera zake ili zishabihiane na Dira hiyo, na Tume ya Kurekebisha Sheria na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanza mchakato wa kupendekeza maboresho ya kisheria yatakayowezesha utekelezaji wa Dira kwa ufanisi.

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akionesha Tuzo ya Heshima na Shukrani aliyopewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
---------------------------------------------
Akizungumzia vipaumbele vya Dira 2050, Rais Samia alisema kwa kuzingatia uwezo wake wa kuzalisha ajira, kuongeza mapato ya Serikali na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine, Dira hiyo imechagua sekta tisa ambazo ni kilimo, viwanda, ujenzi, madini, utalii, uchumi wa buluu, huduma za kijamii, huduma za kifedha, na michezo na ubunifu. Katika hatua nyingine,
Aliagiza kuandaliwa mkakati mahsusi wa mawasiliano na elimu kwa umma kuhusu Dira 2050 ili kuongeza uelewa na ushiriki wa wananchi, huku akisisitiza uwazi katika utoaji wa taarifa za maendeleo ili kuimarisha uaminifu kati ya Serikali na wananchi.
No comments:
Post a Comment