NEWS

Thursday, 3 July 2025

Waziri Mkuu Majaliwa atangaza kung’atuka ubunge Ruangwa



Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Na Mwandishi Wetu

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, jana Julai 2, 2025 alitangaza rasmi kutogombea ubunge katika jimbo la Ruangwa, mkoani Lindi ili kupisha sura mpya kuongoza jimbo hilo.

Majaliwa ambaye kitaaluma ni mwalimu, ameliongoza jimbo la Ruangwa kwa tiketi ya chama tawala - CCM kwa miaka 15 tangu mwaka 2010.

“Asanteni Ruangwa,” ndiyo kauli aliyoitoa Majaliwa wakati akiwaaga wapiga kura wake waliomuunga mkono kwa miaka 15 ya kuwa mbunge wa jimbo hilo la kusini mwa Tanzania.

Jimbo la Ruangwa sasa litashuhudia mchuano wa wanasiasa wengine wanaowania kumrithi Majaliwa ambaye aliingia kwenye ulingo wa siasa baada ya kutumikia ualimu na ukuu wa wilaya.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu mwaka 2015 na Rais wa wakati huo, Dkt. John Pombe Magufuli, Majaliwa alipata kuwa Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Katika uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye kikatiba kama Makamu wa Rais alirithi nafasi ya urais baada ya kifo cha Dkt. Magufuli, Majaliwa alibaki kuwa Waziri Mkuu.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, mteule wa nafasi ya Waziri Mkuu hutokana na mbunge wa jimbo la uchaguzi.

Tangu Tanzania Bara (zamani Tanganyika) ijipatie uhuru wake kutoka kwa Waingereza mwaka 1961, Majaliwa amekuwa Waziri Mkuu wa 11 kushika wadhifu huo mkubwa wa dola.

Baba wa Taifa na gwiji wa siasa barani Afrika, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alikuwa ndiye Mtanzania wa kwanza kushika nafasi hiyo kabla na baada ya uhuru kuanzia Septemba 1960 hadi Desemba 1962.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages