
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Tanzania, Camillus Wambura, akikata utepe kuzindua jengo jipya la Ofisi ya Dawati la Jinsia na Watoto mjini Tarime, mkoani Mara, Juni 24, 2025.
-----------------------------------------
cgmjournalist@gmail.com



Wahanga wa ukatili wa kijinsia, wakiwemo watoto wa kike katika wilaya ya Tarime mkoani Mara, sasa wana kila sababu ya kutabasamu, baada ya Jeshi la Polisi kuzindua jengo jipya la Ofisi ya Dawati la Jinsia na Watoto, litakalokuwa mkombozi na kimbilio la usalama na ulinzi wao.
Kwa mara ya kwanza, jamii ya Tarime inapata kituo cha kisasa chenye watumishi waliopata mafunzo maalum ya kushughulikia kesi za ukatili wa kijinsia kwa weledi na staha.
Uzinduzi wa jengo hilo ni kama taa inayowashwa usiku wa giza nene, ikiashiria kuwa kuna mwanga upande wa pili wa mapambano dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.
Kwa muda mrefu, Tarime imekuwa na doa la minyororo ya kimya ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto wa kike, hasa ukeketaji, ndoa za utotoni na mimba zisizotarajiwa.
Kwa wasichana wengi wa wilaya hii, utu wao umekuwa ukipimwa kwa mapokeo ya mila zilizopitwa na wakati, na hivyo ndoto zao kukatishwa kabla hawajafikia maisha ya utu uzima.
Lakini sasa, kupitia jengo hilo jipya la Dawati la Jinsia na Watoto, umefunguliwa mlango mpya wa matumaini ya ulinzi wa usalama, afya, utu na haki kwa watoto hao na wahanga wengine wa ukatili wa kijinsia.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillus Wambura (katikati waliokaa), kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali mara baada ya kuzindua jengo hilo.
---------------------------------------
Kwa mujibu wa Kamishna wa Pilisi (CP) wa Kamisheni ya Polisi Jamii nchini, Faustine Chilogile, uzinduzi wa jengo hilo ulitanguliwa na ufikishaji elimu ya ukatili wa kijinsia katika kata 60 za Mkoa wa Kipolisi Tarime-Rorya.
Jengo hilo lilizinduliwa Juni 24, 2025 na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini, Camillus Wambura, mjini Tarime, ambapo alisema litakuwa jibu la kilio cha miongo mingi cha wahanga wa ukati wa kijinsia, wakiwemo watoto wa kike ambao wamekuwa wakidhulumiwa, kuumizwa na kukosa mahali pa kueleza machungu yao kwa uhuru na kupata msaada.
"Jengo hili litakuwa kimbilio salama kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia," IGP Wambura alisema katika hotuba yake na kusisitiza kuwa litakuwa ngao dhidi ya ukatili wa kijinsia unaojificha nyuma ya mila na desturi zenye madhara kwenye jamii.
Alisema, kwa mara ya kwanza, Tarime imepata ofisi ya Dawati la Jinsia na Watoto yenye askari polisi waliopata mafunzo maalum kuhusu ukatili wa kijinsia - waliobobea katika kusikiliza, kusaidia na kulinda watoto wa kike na makundi mengine ya jamii dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Mratibu wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Faidha Suleiman, akitoa maelezo kuhusu jengo hilo, mbele ya IGP Camillus Wambura, ndani ya kimojawapo cha vyumba vya jengo hilo.
-----------------------------------------
Jengo hilo limejengwa kutokana na ufadhili uliotolewa na Serikali ya Finland kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), chini ya Programu ya Chaguo Langu, Haki Yangu.
Kwa mujibu wa IGP Wambura, mafanikio ya ujenzi wa jengo hilo yasingepatikana kama si uhusiano wa uliojengwa na Serikali ya Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na mataifa mbalimbali.
Mratibu wa TGNP, Flora Ndaba, alibainisha kuwa ujenzi wa jengo hilo umegharimu shilingi milioni 300, ikiwa ni uwekezaji mkubwa wa kulinda haki za kijinsia kwa wanawake, wanaume na watoto wa kike.

Mratibu wa TGNP, Flora Ndaba, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa jengo hilo.
-----------------------------------------
Dkt. Majaliwa Gerald Marwa kutoka UNFPA Tanzania, alisema ujenzi wa jengo hilo ni uthibitisho wa dhamira ya dhati ya Jeshi la Polisi na Serikali ya Tanzania kwa ujumla katika kulinda haki za wananchi dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Kupitia Dawati hilo la Jinsia na Watoto, wahanga wa ukatili na unyanyasaji wa kijinsia watapewa huduma za kisaikolojia, msaada wa kisheria na ufuatiliaji wa haki zao kwa njia ya kitaalamu na kwa wakati.
Wenyeji wanasema kabla ya ofisi hiyo, visa vya ukatili wa kijinsia vilikuwa vikishughulikiwa katika mazingira yasiyo rafiki.
“Mara nyingi, kesi za ukatili wa kijinsia zilifutwa kimyakimya, au wahusika wakiachwa bila adhabu, huku waathirika wakibaki na aibu na huzuni,” mmoja wa wanamke wakazi wa mjini Tarime aliiambia Mara Online News kwa sharti la kuhifadhiwa jina.
Lakini sasa, hali hiyo inakwenda kubadilika. Jengo hilo la Ofisi ya Dawati la Jinsia na Watoto ni ushahidi kwamba mfumo wa ulinzi na utetezi wa haki za kijinsia wilayani Tarime unaelekea pazuri zaidi.
“Ninashukuru Jeshi la Polisi na Serikali yetu kwa kutuletea ofisi hii ya Dawati la Jinsia na Watoto hapa Tarime, sasa tunajua tukinyanyaswa tuna pa kukimbilia,” alisema msichana mkazi wa mjini Tarime (jina tunalihifadhi), akiitaja ofisi hiyo kama mlinzi wa ndoto za watoto wa kike.
“Sauti ya mtoto wa kike aliyekuwa akilia gizani katika wilaya yetu ya Tarime sasa ina mwanga wa kuitikia,” alisema mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Tatu, mkazi wa mjini Tarime pia.

Askari Polisi, watoto wa kike na wananchi wakiimba na kucheza wakati wa hafla ya uzinduzi wa jengo hilo.
-----------------------------------------
Hakika, kwa watoto wa kike wa Tarime, ofisi hiyo ni zaidi ya jengo. Ni alama ya kutambuliwa, kuthaminiwa, kusikilizwa na kulindwa. Ni kielelezo kuwa Serikali inawajali, inasimama nao na kwamba kilio chao si cha kupuuzwa tena.
Hivyo, kama taifa, sote tunapaswa kusema kwa sauti moja: Kila mtoto wa kike ana haki ya kuishi bila ukatili, hofu na mila kandamizi.
Kama alivyosema IGP Wambura, mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia siyo ya familia pekee, ni jukumu la jamii nzima. Lazima jamii isimame kwa pamoja - polisi, wazazi, walimu, viongozi wa dini na mila, vijana na hata watoto - kupiga vita ukatili huo kwa vitendo.
Kwa mfano, iwapo mzazi atachukua hatua ya kuripoti mpango wa kumuozesha mtoto wa kike, au mwalimu akagundua dalili za mimba kwa mwanafunzi na kuripoti haraka, basi Dawati hilo la Jinsia na Watoto litaweza kuchukua hatua mapema kabla madhara hayajatokea.
Kwa hiyo, matarajio ni kwamba miaka michache ijayo, Dawati la Jinsia na Watoto Tarime litaweza kusimulia mabadiliko chanya kuhusu wahanga wa ukatili wa kijinsia, wakiwemo watoto wa kike waliopona majeraha ya ukatili huo, waliopata haki zao, waliosimama kuwa wanawake na wanaume jasiri, walimu, viongozi na hata askari polisi watetezi wa haki za wengine.
No comments:
Post a Comment