India imesitisha uagizaji wa karibu vifaa nusu milioni vya kupimia virusi vya corona kutoka China baada ya kubainika kuwa vifaa hivyo ''Vina dosari''.
Mji wa Delhi pia umeondoa vifaa ambavyo tayari vilikuwa vinatumika katika majimbo kadhaa.
Vifaa hivyo huchukua muda wa karibu dakika 30 kutoa majibu. Hutumiwa kusaidia maafisa kuelewa hali ya maambukizi katika eneo fulani.
China imekasirishwa na madai ya India.
''Ubora wa vifaa tiba kutoka China ni jambo linalopewa kipaumbele. Si haki kwa watu fulani kuita vifaa vitokavyo China kuwa vyenye ''dosari'' alieleza msemaji wa ubalozi wa China Ji Rong katika taarifa yake siku ya Jumanne.
Vifaa hivi vya upimaji haviwezi kupima virusi vya corona vyenyewe na wanasayansi kadhaa wameeleza kuhusu matumizi yake katika kubaini ugonjwa.
Majimbo kadhaa nchini India yamekuwa yakishinikiza baraza la utafiti(ICMR) nchini humo kuruhusu vipimo kwa kutumia vifaa hivyo kutokana na madai kuwa India haifanyi jitihada za kutosha. Awali ICMR ilikua ikikataa, lakini ilifungua milango, kuingiza vifaa vya upimaji kutoka kwa makampuni mawili ya nchini China.
Hatahivyo, muda mfupi baada ya majimbo kadhaa kuanza kulalamika kuwa vifaa hivyo vya kupimia vina uhakiki wa 5% pekee, yakiongeza kuwa yalivitumia kwa wagonjwa ambao tayari walishafahamu kuwa wana maambukizi , lakini majibu yalionekana hawajaambukizwa.
Pia vifaa hivyo vilishindwa upande wa jaribio la ubora wake lililofanywa na ICMR.
Siku ya Jumatatu, suala hilo lilikuwa na changamoto zaidi baada ya mahakama ya juu ya mjini Delhi kutoa uamuzi kuhusu gharama za vifaa hivyo ikisema kuwa serikali imetumia pesa nyingi.
Hatahivyo, maafisa wameviambia vyombo vya habari nchini humo kuwa serikali ''haitapoteza hata rupia moja'' kwa kuahirisha kuagiza vifaa hivyo kwa kuwa hawajailipa China malipo ya awali, na kufunga kabisa zoezi la uingizaji wa vifaa hivyo nchini India.
Nchi nyingine kadhaa zimeripoti tatizo kama hilo kwa vifaa kutoka China, lakini Beijing imekana kuhusu madai ya vifaa vyake kutokuwa na ubora.
Nchini Marekani, gazeti la New York Times liliripoti kuwa vifaa vya kupimia ambavyo''kwa kweli havina ubora'' vimefurika katika soko la nchini Marekani, likisema kuwa vifaa hivyo vimekuwa vikitoa majibu kimakosa kuwa hawajaambukizwa wakati ukweli ni kuwa wana maambukizi.
Nchini Uingereza, wanasayansi walilalamikia ufanisi wa vifaa hivyo na Waziri wa Afya Matt Hancock aliviambia vyombo vya habari kuwa vifaa hivyo ''havina ubora wa kutosha''
Kwa sasa inaonesha kuwa vipimo vya maabara, ambavyo vina mchakato mrefu na vyenye kuchukua muda mrefu, bado ni njia pekee ya kuaminika.
Kanuni ni rahisi sana - kipimo kinaegemea katika kuangalia ni msingi wa kuangalia kinga ya mwili dhidi ya Covid-19 kutoka kwenye sampuli za damu.
Kimefananishwa na namna ya kipimo cha ndio au hapana cha kipimo cha ujauzito.
BBC Swahili
No comments:
Post a Comment