Katibu Mkuu Wizara ya
Kilimo, Gerald Musabila Kusaya amesema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa
jengo la Wizara ya Kilimo linalojengwa viwanja vya nane nane nyakabindi Bariadi,
Simiyu.
Aidha Kusaya amemtaka
mkandarasi ambaye ni Suma JKT kuhakikisha ujenzi unakamilika kabla ya Mei
30, 2020.
Ujenzi wa jengo hilo ulianza mwaka jana 2019 na lilitakiwa kukamilika machi 30 na hadi sasa limefikia asilimia 70 ya ujenzi huku changamoto ikitajwa kuwa ni mabadiliko ya mchoro.
Katika hatua
nyingine katibu mkuu huyo amewahakikishia wanunuzi wa pamba, viongozi wa
chama na serikali mkoani Simiyu kuwa madeni yote yatalipwa kabla ya msimu mpya
haujaanza.
Ameyasema hayo leo kwa nyakati tofauti kwenye ziara yake ya siku moja mkoani hapo iliyokuwa na lengo la kuangalia maandalizi ya ufunguzi wa maonyesho ya wakulima kitaifa (Nanenane) na alipotembelea kiwanda cha kuchambua pamba cha alliance kilichopo wilayani Bariadi.
Amesema kuwa serikali haitatangaza kuanza kwa msimu mwingine wakati bado kuna wakulima wanadai, nakuongeza kuwa wanafanya jitihada zote kuhakikisha wakulima wanalipwa ikiwa ni pamoja na ushuru mwingine wote ukiwemo wa halmashauri na Amcos.
" Yapo mazungumzo yanaendelea, niwahakikishie kuwa deni lote litalipwa hatutangia kwenye msimu mpya wakati bado kuna wakulima wanadai pesa zao za msimu uliopita,"alisema Kusaya.
Anthony Mtaka ni mkuu wa mkoa huo amesema jumla ya madeni yote ni kiasi cha shilingi bilioni 8.9 huku wakulima peke yao wakidai zaidi ya bilioni 3, na kiasi kingine kilichobaki kikiwa madeni ya halmashauri na Amcos.
"zaidi ya wakulima 7000 katika Mkoa huo bado wanadai hela ya pamba yao, kilo milioni 2.6 za pamba zinadaiwa alisema Mtaka na kuongeza kuwa:
"Wizara ya kilimo ni vema mkafanya utafiti wa kina kwanza kabla ya kutangaza bei elekezi ya pamba, "aliongeza Mtaka
Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu Enock Yakobo ameitaka serikali kutimiza ahadi hiyo huku akiongeza kuwa kila wakiingia vijiji jambo linalozungumzwa na wakulima ni madeni ya pamba na hivyo kuitaka serikali kulilipa kabla ya kuingia kwenye uchaguzi mkuu.
Awali akisoma
taarifa katibu wanunuzi wa pamba nchini Boaz Ogolla alisema
kuwa kabla ya kuanza msimu wa ununuzi uliopita walikaa vikao mbalimbali na serikali
na kuwekeana makubaliano ya jinsi ya kununua pamba.
Ogolla alisema bei
ambayo ilitangazwa na serikali haikuendana na bei ya soko la dunia hali ambayo
ilikuwa ikiwangiza katika hasara lakini serikali iliwahidi kuwa itafidia hasara
ambayo itatokea kutokana na bei katika soko la dunia kushuka huku ikiwasisitiza
wanunuzi waendelee kununua kwa bei ambayo ilikuwa imetengazwa.
" Wanunuzi tulitii hilo agizo, na kununua pamba kwa hasara, tukiwa na imani kuwa serikali itatekeleza ahadi yake ya kufidia hasara ambayo tulipata, na kweli wanunuzi waliuza kwa hasara tunaomba serikali itufidie hiyo hasara," alisema Ogolla.
Madeni hayo ni ya msimu uliopita 2018/19 ambayo yanahusisha madeni ya wakulima , ushuru wa halmashauri, mfuko wa kuendeleza zao hilo (CDTF) pamoja na ushuru wa chama vya msingi vya ushirika vya msingi( Amcos )
(Habari na Anita Balingilaki, Bariadi - Simiyu)
No comments:
Post a Comment