NEWS

Wednesday 20 May 2020

CRDB yaanza kuwezesha malipo ya fidia Nyamongo, mawaziri washuhudia


BENKI ya CRDB imeahidi kuendesha huduma bora za kifedha kwa wanufaika 1,639 wa malipo ya fidia kupisha mradi wa uchimbaji madini katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaoendeshwa na kampuni ya Barrick katika eneo la Nyamongo wilayani Tarime, mara.
Waziri wa Madini, Dotto Biteko

Mkurugenzi wa Wateja Wadogo wa Benki ya CRDB, Boma Raballa, ameyasema hayo leo Jumatano Mei 20, 2020 mbele ya Waziri wa Madini, Dotto Biteko, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira, Mussa Azzan Zungu na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Angeline Mabula katika hafla ya uzinduzi wa malipo ya fidia hizo.

 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Azzan Zungu
Aidha, Raballa ameishukuru serikali kwa kuiamini CRDB na kuishirikisha kwenye mpango huo, ambapo amesisitiza kuwa benki hiyo imejipanga kuhakikisha utekelezaji wake unakidhi matarajio chanya ya pande zote.

“Ili mpango huu wa ulipaji fidia uweze kufanikiwa, jambo kubwa ni kutoa elimu ya kifedha kwa wananchi na kuweka mifumo madhubuti ya malipo kama vile miundombinu ya huduma bora za kifedha,” amesema mkurugenzi huyo.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula
 Amesema katika tathimini ya awali imeonesha wanufaika wengi wa malipo ya kupisha mradi huo wa madini hawana akaunti za benki na wana uhitaji mkubwa wa elimu ya fedha kwa matumizi ya fedha.

“Hivyo sisi kama taasisi ya fedha, mkakati wetu wa kwanza tuliokuja nao ni kuanza kutoa elimu ya matumizi bora ya fedha na tunaendesha kazi ya ufunguaji wa akaunti kwa wakazi zaidi ya 2,000. Tunafanya kupitia tawi letu linalotembea (mobile branch) ambalo litakuwa hapa,” amesema Raballa na kuongeza:


“Ufanikishaji wa kazi hii ya ufunguaji wa akaunti utasaidia wananchi wote kupokea malipo yao kwa uharaka katika njia usalama na kuepuka madhara yanayoweza kuambatana na kukaa na fedha taslimu majumbani kwao, lakini pia wateja wote watakaofungua akaunti wataunganishwa na huduma za simu benki na simu akauti ambazo zitawawezesha kufanya miamala ya kifedha popote pale walipo.”
 
Mkurugenzi wa Wateja Wadogo wa Benki ya CRDB, Boma Raballa
Raballa ameongeza kuwa pamoaja na mkakati wa kutumia tawi linalotembea na CRDB Wakala, benki hiyo tayari imefanya upembuzi yakinifu wa kufungua tawi rasmi mjini Nyamongo na kwamba ujenzi huo utaanza na tawi hilo kufunguliwa rasmi ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa.

“Tunatumaini kuwa si tu tawi hilo litaongeza wigo wa upatikanaji huduma kwa wanufaika au wakazi wa Nyamongo, bali litachochea na kukuza shughuli mbalimbali za kiuchumi kupitia mikopo na huduma nyingine nyingi zinazotolewa na CRDB, hivyo niwasihi Wananyamongo tukae mkao wa kula,” amesema Raballa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages