NEWS

Saturday 30 May 2020

Herd immunity inavoweza kupunguza maambukizi ya Corona




WAKATI  bhaadi ya watu duniani wapo kwenye zuio la kutoka ndani ya nyumba zao, takwimu zinaonesha mpaka sasa vifo vinavyotokana na virusi vya corona ni mara 10 ya vile vilivyosababishwa na homa nyingine za mafua ikiwemo SARS na MERS.

Wanasayansi na watafiti wanahangaika kuhakikisha kwamba wanasaidia dunia kurudi kwenye hali ya kawaida kwa kugundua chanjo itayotukinga dhidi ya corona, ukiacha njia zisizohusisha dawa ama zile za muda mfupi kama vile kunawa mikono, kuvaa barakoa na kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu una mtu.

Chanjo ya maabara ina hatua nyingi za kitafiti kabla ya kukubalika kwamba ni salama kwa matumizi ya binadamu na mpaka sasa taarifa zinaonesha upatikanaji wake ni kuanzia mwisho wa mwaka huu.

Kwa kulitambua hili, kuna nchi kama Sweden zimeamua kutegemea kinga ya jumla ya mwili ijulikanayo kitaalamu kama “herd immunity” kama njia mojawapo ya kupambana na janga la corona mpaka pale chanjo itakapopatikana.

Wao hawajaweka nchi yao kwenye zuio la raia wao kutoka ndani ya nyumba zao, lakini wananchi wanatakiwa kufuata ushauri wa kitaalamu kuzuia maambukizi huku wale walio kwenye hatari zaidi ya kupata maambukizi ya corona wakiwamo wazee na wenye magonjwa suku wakihimizwa kukaa nyumbani.

Hata kabla ya ujio wa virusi vya corona, aina hii ya kinga imetumika/kuhusishwa na hatua za kumudu magonjwa mengine ya kuambukizwa ikiwemo polio, surua, tetekuwanga, n.k.

Sasa tuangalie ni kwa namna gani kinga hii ya jumla inafanya kazi katika jamii.

Kinga ya jumla ya mwili ni nini?

Virusi vya SARS-CoV-2 vinavyosababisha corona vilipoanza kusambaa hakuna mtu aliyekuwa na kinga dhidi yake, hivyo havikupata upinzani wowote kuingia kwenye mwili wa binadamu hali iliyovifanya kusambaa kwa haraka.

Watu wengi wanapoendelea kuambukizwa, wengine hutengeneza kinga dhidi ya virusi hivi na idadi ya walioambukizwa na waliotengeneza kinga wanapoongezeka basi jamii nzima inapata kinga na hii ndio hujulikana kama kinga ya mwili ya jumla kitalaamu Herd Immunity.

Kinga hii ya jumla ya mwili inapatikana pia pale ambapo watu wengi kwenye jamii wamepata chanjo na hivyo kutengeneza kinga dhidi ya ugonjwa fulani ila kwa sasa haiwezekani kwa kuwa chanjo ya virusi vya corona bado haijapatikana.

Taarifa za awali za kisayansi zinatuonesha kwamba iwapo asilimia 70 ya watu watapata maambukizi ya virusi vya corona na kutengeneza kinga basi asilimia thelathini waliobaki watakingwa pia.

Swali lako msomaji hapa litakuwa - hii inawezekana vipi?

Unaposema asilimia 70 inamaana kwamba ukiwa na watu saba kati ya 10 wameambukizwa na wana kinga inamaana usambazaji wa virusi utapungua maana hata kama watakuwa katika hatari ya kupata virusi vya corona hawatapata maambukizi na wasipopata nao hawataweza kuambukiza wale watatu waliobaki ambao hawana kinga, hivyo kusimamisha mzunguko wa maambukizi.

Changamoto ya aina hii ya kinga wakati chanzo za maambukizi ni kirusi ni kwamba virusi vina tabia ya kubadilika vinasaba vinavokitengeneza na kuwa kipya kabisa.

Hivyo basi, kinga zake zinakuwa za muda mfupi na kinga ya aina moja ya kirusi haimaanishi ni kinga ya aina nyingine ya kirusi hata kama ni familia moja.

Mfano, mtu aliyepata kinga dhidhi ya SARS-CoV inayosababisha SARS haimkingi mtu na SARS-CoV-2 ingawa virusi vyote vinatoka kwenye familia ya corona.

Kupitia tafiti inaonekana wazi kwamba kinga ya kawaida ya mwili dhidi ya homa, mafua bila chanjo inadumu chini ya mwaka mmoja. Iwapo kinga dhidi ya virusi vya corona ni kama hizi basi inatarajiwa kwamba kinga hii itadumu kwa miezi kadhaa au miaka lakini sio kwa maisha yote, hivyo kuongeza umuhimu wa kupatikana kwa chanjo.

Tutarajie nini miezi ijayo?

Wanasayansi wanafanya kazi usiku na mchana ili chanjo ipatikane na watu wapate kinga dhidi ya virusi vya corona.

Wakati tukisubiria upatikanaji wake, kila mmoja wetu afanye sehemu yake kuhakikisha usalama wake binafsi, usalama wa familia yake na Tanzania yetu. Sote kwa jumla tuchukue tahadhari kama tunavyoshauriwa na wataalamu wa afya.

Na Daktari Shally Zumba Mwashemele

Simu: +255 716 615 651 Barua Pepe: shallyzumba@gmail.com

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages