Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini |
Akizungumza na waandishi wa habari
Mei 23, 2020, Katibu Tawala wa mkoa huo, Jumanne Sagini amesema serikali
mkoani humo imejipanga pia kutumia vizuri siku 28 zilizotolewa na wizara yenye
dhamana ya elimu kufanya maandalizi ya mtihani wa taifa wa kidato hicho
utakaoanza Juni 29, 2020.
“Elimu ni kipaumbele cha kwanza mkoani kwetu, tumejipanga kikamilifu kuwapokea vijana wetu wa kidato cha sita, tuliandaa mkakati wa kuwasaidia kujisomea wakati wa likizo ya tahadhari ya corona,” amesema Sagini na kuongeza:
“Viongozi katika maeneo yote watahakikisha tahadhari zote zinazotolewa na wizara yenye dhamana na afya katika kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona yanazingatiwa.”
Ametoa wito kwa wazazi na walezi mkoani humo kuendelea kusimamia na kuhimiza watoto ambao bado wako likizo ya dharura kujisomea mpaka shule zitakapofunguliwa.
Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Mwalimu Ernest Hinju, amesema kipindi hiki cha likizo ya dharura wanafunzi wamekuwa wakijisomea, kufanya majaribio na kurudia mada ambazo hazikueleweka vizuri.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Fabian Manoza, amesema wamejipanga kuhakikisha wanakamilisha kwa wakati mahitaji yote ya kimasomo kwa wanafunzi wa kidato cha sita kuwawezesha kujiandaa kwa ajili ya mtihani wa taifa.
Mkoa wa Simiyu una wanafunzi 953 wanaotarajiwa kufanya mtiani wa kuhitimu kidato sita kuanzia June 29, 2020.
(Imeandikwa na Anita Balingilaki, Simiyu)
No comments:
Post a Comment