CHAMA
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) sasa kimebaki historia wilaya ya Tarime
baada ya Katibu wake, Samwel Mgaya kufuata nyayo za Mwenyekiti wake, Mwita
Joseph kukihama na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kwa
hatua hiyo, ni wazi kwamba Chadema sasa kimebaki bila mwenyekiti na katibu wa
wilaya ya Tarime mkoani Mara.
Mgaya
ametangaza kuhamia CCM leo Mei 25, 2020 ikiwa ni takriban mwezi umepita tangu
Joseph atimkie kwenye chama hicho tawala kwa maelezo ya kutoridhishwa na
mwenendo wa uongozi wa juu wa Chadema.
Akizungumza
mbele ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime, Daudi Ngicho na Naibu Waziri
mwenye dhamana ya Tamisemi, Mwita Waitara, Mgaya amesema ameamua kuhamia chama
hicho tawala kwa hiari yake.
“Nimetafakari…
nimekuja kuungana nanyi [CCM] kumuunga mkono Rais John Magufuli, mambo
[akimaanisha maendeleo] anayofanya sasa hivi hata kama ni mtoto mdogo
anayaelewa,” amesema Mgaya.
Akizungumza
wakati wa mapokezi hayo ofisini kwake mjini Tarime, Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Ngicho,
amesema Mgaya na Joseph ni wapiganaji wazuri na amewakaribisha kuungana na
wanachama wa chama hicho katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya Watanzania.
Samweli Mgaya (katikati) akiwa amevalia sare za CCM mara baada ya kujiunga na chama hicho. Kulia ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Daudi Ngicho na kushoto ni Katibu wa chama hicho wilayani, Hamis Mkaruka. |
Naye
Naibu Waziri Waitara ambaye pia ni Mbunge wa Ukonga mkoani Dar es Salaam, amesema
CCM kimepata watu muhimu [Joseph na Mgaya] na kutuma salamu kwa Chadema kwamba
kitarajie kuporomoka zaidi.
“Watu
wametambua kazi nzuri inayofanywa na Rais Dkt John Magufuli, malalamiko mengi ya
wananchi yameshughulikiwa, hii ni serikali sikivu,” amesema Waitara.
Naibu Waziri wa TAMISEMI na kada wa CCM, Mwita Waitara akisisitiza jambo wakati wa mapokezi ya Katibu wa Chadema Wilaya ya Tarime, Samwel Mgaya (hayupo pichani) |
Wengine
walioungana na Mgaya kuhamia CCM leo, vyama na kata wanakotoka wilayani Tarime
vikiwa kwenye mabano ni Nashon Mchuma (Chadema, Gwitiryo), Boniphace Mataro
(Chadema, Matongo), Emmanuel Marwa (Chadema, Nyamwaga) na George Nyanchama (ACT
– Wazalendo, Nyandoto).
Hata
hivyo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mara, Lucas Ngoto amesema chama hicho kiko
imara kwani wanaohama ni viongozi lakini wanachama wapo wengi wanaoweza kuziba
nafasi za uenyekiti na ukatibu zilizoachwa wazi wilayani Tarime.
(Imeandikwa na
Waitara Meng’anyi, Tarime)
No comments:
Post a Comment