NEWS

Monday 29 June 2020

Familia zinavyochangia ukatili wa kingono kwa watoto

IMEELEZWA vitendo vya ukatili wa kingono dhidi ya watoto kwa kiasi kikubwa vinachangiwa na wazazi wasiozingatia malezi ya kimaadili katika familia zao, lakini pia wanafamilia kutovipa ushirikiano vyombo vya sheria katika kesi za wanaotenda ukatili huo.
Anita Dotto akizungumza na mwandishi wa makala hii

Kwa mujibu wa watetezi wa haki za binadamu, vitendo vingi vya ukatili wa kingono kwa watoto vinafanywa na baadhi ya wanafamilia husika.

Mapungufu hayo ya kifamilia yameendelea kutoa mwanya kwa watu wazima walioporomoka kimaadili kufanya ukatili wa kingono dhidi ya watoto na kukwepa mkono wa sheria.

Matokeo yake baadhi ya watoto waliotendewa ukatili huo huishia kukosa haki zao licha ya vitendo hivyo kuwaathiri kimwili, kiakili na kisaikolojia kama si kuwaharibia mustakabali wa maisha yao ya baadaye.

“Mara nyingi ukatili wa kingono kwa mtoto unafanywa na watu wa karibu na mtoto, siyo watu wa mbali,” anasema Sheikh Eliasa Abeid, mjumbe wa dawati la utetezi wa haki za binadamu lililopo Igombe, kata ya Bugogwa wilayani Ilemela, Mwanza.

Abeid aliyezungumza na Mara Online News wilayani Ilemela jana (Juni 28, 2020), anasisitiza kuwa wazazi wa zama hizi ni kisababishi kikuu cha visa vya ukatili huo katika jamii.

“Baadhi ya familia zinaishi katika mazingira amabayo watoto wanakuwa hawana malezi mazuri, unakuta saa mbili za usiku watoto hawapo majumbani, watoto wa kike wanatembea ovyo, muda waliotakiwa kuwa nyumbani wanajisomea na kufanya kazi unakuta wako kwenye madisko.

“Kwamba wazazi wa sasa tunawalea watoto kidijitali, yaani kiusasa zaidi, mtoto anakuwa na uhuru uliopitiliza, hakanywi, hafokewi na haelekezwi, na hayo mazingira mtoto anaanza akiwa na miaka mitano mpaka kukua.

“Matokeo yake anakuwa mtoto wa ovyo, hawezi kudhibitiwa, mwishowe anajiingiza kwenye vitendo visivyofaa mpaka anafanyiwa ukatili wa kingono,” anasema Abeid ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Kitaifa la Waislamu Tanzania (Bakwata) Kata ya Bugogwa na mwakilishi wa taasisi hiyo ya dini kwenye dawati la utetezi wa haki za binadamu Igombe.

Mwenyekiti wa dawati hilo, Mwalimu Mashaka Musiba, anasema eneo hilo limekuwa na matukio mengi ya ukatili wa kingono kwa watoto kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu kutoka sehemu mbalimbali kwa ajili ya shughuli za uvuvi katika Ziwa Victoria.
Mwalimu Mashaka Musiba

“Kata ya Bugogwa, hususan hapa Igombe ni eneo la uvuvi, kuna mwingiliano mkubwa wa watu wanaotoka mila na desturi tofauti, watu wanakuja na tabia nyingine ambazo ni hatarishi,” anasema Musiba na kuendelea:

“Kwa hiyo vitendo vya ukatili wa kingono kwa watoto wenye umri chini ya miaka 18 vipo, tunashirikiana na Jeshi la Polisi kuchukua hatua lakini baadhi ya kesi zinafeli kutokana na upande wa mtoto aliyefanyiwa ukatili kutokwenda kutoa ushahidi mahakamani, hivyo baadhi ya kesi kuishia kufutwa.”

Mwalimu huyo wa Shule ya Msingi Kisundi wilayani Ilemela, anatoa mifano kadhaa ya visa vya ukatili wa kingono kwa watoto vilivyotokea katani Bugogwa ukiwamo wa mwanafunzi aliyepewa ujauzito na baba yake wa kufikia.

“Binti huyo ilikuwa amalize darasa la saba mwaka huu (2020), lakini alipewa ujauzito na baba wakambo yake,” alisema Mwalimu Musiba na kuendelea:

“Kilichofanyika mama yake alimpeleka kimya kimya kupima ujauzito kwenye kituo cha afya, baada ya kugundulika ana ujauzito, badala ya kupeleka taarifa hizo shuleni hatua zianze kuchukuliwa, alirudi nyumbani akaanzisha ugomvi na mume wake, kuona hivyo mume wake huyo akatoroka.

“Jamaa anatafutwa mpaka leo haijulikani yuko wapi, ingawa tunakuwa hatuamini siri iliyopo, inawezekana mama alimwambia ili kumsaidia aweze kukimbia. Basi taratibu zikafuatwa mtoto akasimamishwa masomo, ilikuwa mwaka jana (2019) na binti yule atakuwa ameshajifungua.”

Mwalimu Musiba alitaja kisa kingine kuwa ni cha mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Bugogwa mwenye umri wa miaka tisa aliyenusuriwa kubakwa wakati wa likizo ya dharura ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona (COVID-19).

“Mtoto huyo alidanganywa na kijana fulani, kesi yake iko mahakamani, jamaa alikuwa anajaribu kumbaka, majirani wakashtukia lile dili wakapiga kelele akakamatwa,” anasema.

Mwenyekiti huyo wa dawati la utetezi wa haki za binadamu kata ya Gugogwa anataja tukio jingine kuwa ni la mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kayenze Ndogo, mwenye umri wa miaka 16 aliyefichwa siku mbili mfululizo na kijana mwenye umri wa miaka 25.

“Huyo binti alipotea nyumbani kwa siku mbili, kisha ikagundulika alikuwa amefichwa ndani na kijana huyo kule Kayenze Ndogo jirani na Igombe, suala lake nalo liko mahakamani linashughulikiwa. Kwa hiyo changamoto kama hizi zipo, nafikiri sasa shule zinapofunguliwa ndio tutajua kesi nyingi zaidi,” anasema Musiba.

Naye Sheikh Abeid anasema mtoto mwingine wa darasa la pili aliyebakwa katani humo mwaka 2017 nusura kesi hiyo ihujumie na ndugu wa mbakaji.
 
Sheikh Eliasa Abeid
“Kipindi cha kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Ilemela, wazazi wa vijana waliomkamata mbakaji wa mtoto yule walitaka kupenyeza visenti ili wale vijana wasiende kutoa ushahidi.

“Uzuri wale vijana ni Waislamu, hivyo nilimwagiza imamu wa msikiti wa lile eneo akawaita tukawambia kama hawakutoa ushahidi kwa mujibu wa aya na hadithi ni kosa gani watakalokuwa wamefanya, na wao watakuwa wameshiriki kitendo cha kuzini na mtoto yule.

“Tukawaelimisha kwa mambo ya kidunia watakuwa wamefanya kosa gani, lakini kidini watakuwa wamefanya kosa gani, wakatuelewa wakakubali kutoa ushahidi.

“Tukaenda mbali zaidi, tukawashikisha masahafu tukawaapisha ili tuamini kwamba hawatatugeuka, kweli wakaenda wakatoa ushahidi na yule bwana [mbakaji] akafungwa miaka 30, ingawa baadaye alikata rufaa katika mazingira ambayo hatujui akawa ameachiwa na jaji.

“Kwa hiyo, changamoto huwa zipo za watu kugoma, hasa wazazi husika kupewa pesa lakini huwa tunajaribu kupambana nazo,” anaeleza Abeid.

Watetezi wa haki za binadamu wanasisitiza kuwa bado kikwazo kikuu cha mapambano dhidi ya ukatili wa kingono kwa watoto ni baadhi ya wanafamilia kutojitokeza kutoa ushahidi kwenye vyombo vya sheria ili wahusika watiwe hatiani na kuadhibiwa kulingana na makosa waliyotenda.

“Ushahidi umekuwa ukikosekana na watoto wengine wanatoroshwa na wazazi, watuhumiwa wanatoroka,” anasema Anita Dotto, Mwanasheria wa Shirika la Wadada Solutions and Gender Based Violence linalopiga vita ukatili wa kijinsia na kingono kwa watoto mkoani Mwanza ilipo wilaya ya Ilemela.

Dotto anaongeza “Sababu nyingine kubwa ya ukatili wa kingono kwa watoto ni ukosefu wa maadili, ukosefu wa hofu ya Mungu, elimu ya jinsia na athari za ukatili huo na ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi. Tumekuwa tukipaza sauti kwamba familia ndio sehemu salama kwa mtoto, lakini tumegundua ukatili mwingi unafanywa na wanafamilia.”

Kutokana na hali hiyo, mwanasheria huyo anatumia nafasi ya mazungumzo na Mara Online News kutoa mwito kwa jamii kutambua kuwa mlinzi wa mtoto ni jamii nzima.

“Sisi wote tunahusika katika ulinzi wa mtoto, tumlinde mtoto dhidi ya vitendo vyote vya ukatili, na kingine, tuwaruhusu watoto wetu kupata elimu kuhusiana na masuala ya afya ya uzazi,” anasema Dotto na kuendelea:

“Wazazi wengi wanazuia watoto wao wakidai hawajakua, lakini ukatili wa kingono unatendeka sana kuanzia watoto wa miaka tisa hadi 14, hapo wanakuwa hawajielewi, kila wanachoambiwa wanasema ndio.

“Lakini mtoto angepata elimu hiyo (ya afya ya uzazi) na ya kujikinga na vitendo vya ukatili angejua mwili wake hautakiwi kuchezewa na mtu mwingine, angejua hatakiwi kujihusisha na vitendo vya ngono.

“Hivyo wazazi wapate nafasi ya kuongea na watoto wao juu ya mambo hayo, na watoto watambue huu ni wakati wao wa kuwa shule, wanatakiwa kujiepusha na vitendo vya ngono, wajue COVID-19 imekuja lakini sio mwisho wa maisha, inaondoka na wanarudi shule, kufanya mapenzi ni kuharibu maisha yao.”

Naye Sheikh Chitambala anatoa mwito akisema “Kwanza, wazazi tuishi na watoto kimaadili kwa sababu tunatarajia wawe watoto wema ili baadaye sisi tukishakuwa wazee wawe watu wazima wema watusaidie.

“Pili, watu wazima wanaopenda kuwafanyia watoto ukatili, wakumbuke kwamba mtoto wa mwenzako ni mtoto wako, jinsi ambavyo wewe mtu mzima huwezi kufurahia mtoto wako kufanyiwa ukatili, pia usiende kumfanyia ukatili mtoto wa mwenzako.”

Ukatili wa kingono kwa watoto pia unapigwa vita na Boresha Project chini ya Ushirikiano wa Kiimani Tanzania (The Tanzania Interfaith Partnership Association - TIP) unaoundwa na taasisi nne za kidini.
Taasisi hizo ni Baraza la Wakristo Tanzania (CCT), Baraza la Kitaifa la Waislamu Tanzania (BAKWATA, Baraza la Maaskofu Wakatoliki Tanzania (TEC) na Ofisi ya Mufti wa Zanzibar (MoZ).

Maono ya TIP ni kutengeneza mtandao thabiti wa kiimani unaochangia uwepo wa jamii ya Kitanzania yenye afya na kizazi kisicho na Ukimwii.

(Imeandikwa na Christopher Gamaina, Ilemela)

2 comments:

  1. Kazi nzuri acha tuendelee kupaza sauti juu ya watoto na kuwakinga na vitendo vya ukatili hususan wa kikngono.

    ReplyDelete
  2. Kazi nzuri acha tuendelee kupaza sauti juu ya watoto na kuwakinga na vitendo vya ukatili hususan wa kikngono.

    ReplyDelete

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages