TAUSI
ambao Rais Dkt John Magufuli alimpatia mjane wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Nyerere, Mama Maria Nyerere, wamewasili salama nyumbani kwa mama huyo Mwitongo,
Butiama mkoani Mara.
Akizungumza
kwa niaba ya Mama Maria Nyerere, mtoto wa Baba wa Taifa, Madaraka Nyerere,
amewambia waandishi wa habari nyumbani hapo leo Juni 2, 2020 kwamba ndege hao
walipokewa Mwitongo Jumapili Mei 31, 2020 kutoka kwa Dkt Gabriel Nyanda wa
Ikulu.
Itakumbukwa
kwamba Jumamosi Mei 30, 2020 katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, Rais
Magufuli alimzawadia Mama Maria Nyerere tausi 25, sambamba na marais wastaafu,
Ali Hasan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete ambao pia walizawadiwa kila
mmoja tausi 25 kwa ajili ya kupendezesha bustani zao.
Mtoto wa Baba wa Taifa, Madaraka Nyerere akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) kuhusu tausi waliopokewa Mwitongo |
“Nawasilisha
shukurani za dhati kwa Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli kwa uamuzi wake wa
kutoa zawadi ya tausi 25 kwake Mama Maria. Narudia salamu za shukurani za Mama
Maria, familia ya Mwalimu Nyerere na ukoo wa Mtemi Nyerere Burito kwa Rais
Magufuli kwa kutoa zawadi hii kubwa na kuwezesha eneo hili la Mwitongo
kuendelea kuboresha historia ya Mwalimu Nyerere,” amesema Madaraka.
Katika
hatua nyingine, Madaraka ametangaza kufunguliwa kwa mapokezi ya watalii katika
eneo la Mwitongo lililokuwa limefungwa tangu Aprili 2020 kwa ajili ya kuchukua
tahadhari dhidi ya kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona (COVID 19).
“Sasa
hivi eneo hili limefunguliwa tena na tunawakaribisha wageni kuja kujifunza
machache juu ya historia ya Mwalimu Nyerere na kushuhudia zawadi ya tausi
iliyotolewa na Mheshimiwa Rais,” amesema mtoto huyo wa Baba wa Taifa.
Madaraka
amesema wanaendelea kuzingatia tahadhari zinazotolewa na wizara ya afya katika
kuzuia maambukizi ya COVID 19 na amewaomba wageni watakaozuru eneo hilo kuvaa
barakoa.
(Imeandikwa na
Christopher Gamaina, Butiama)
No comments:
Post a Comment