WANACHAMA 468 wa CCM wakiwamo
wanaume 434 na wanawake 34 wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania ubunge katika
majimbo 10 ya uchaguzi yanayounda mkoa wa Mara, huku 10 kati yao wakishindwa
kurejesha fomu zao hadi pazia la shughuli hiyo linafungwa jana Julai 17, 2020.
Majimbo yanayounda mkoa wa Mara ni
Musoma Mjini, Musoma Vijijini, Tarime Mjini, Tarime Vijijini, Serengeti, Rorya,
Butiama, Bunda Mjini, Bunda Vijijini na Mwibara.
Kanali mstaafu Kichonge Mahende, mwania ubunge Tarime Mjini |
Kwa mara ya kwanza katika historia
ya mkoa wa Mara kama si Tanzania, Jimbo la Bunda Mjini limeongoza kwa kuwa na
idadi kubwa ya wanachama wa CCM waliojitokeza kuwania nafasi ya ubunge.
Katibu wa CCM Mkoa wa Mara, Shaibu
Ngatiche, ameiambia Mara Online News kwa njia ya simu jana jioni kuwa makada wa
chama hicho waliochukua na kurejesha fomu za kuwania ubunge katika Jimbo la
Bunda Mjini ni 74, wakifuatiwa na Jimbo la Musoma Mjini (64).
Stephen Wasira(kushoto), mwania ubunge Bunda
Mjini
Ngatiche ametaja majimbo mengine na
idadi ya waliochukua fomu za kuwania ubunge ikiwa kwenye mabano kuwa ni
Serengeti (59), Butiama (59), Rorya (52), Mwibara (40), Musoma Vijijini (35),
Bunda Vijijini (31), Tarime Vijijini (30) na Tarime Mjini (25).
Aidha, Ngatiche amesema wanawake 44
walijitokeza kuchukua fomu za kuwania Ubunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara
kupitia Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT), 13 kupitia Umoja wa Vijana wa Chama
Cha Mapinduzi (UVCCM) na mmoja kupitia Jumuiya ya Wazazi ya chama hicho.
No comments:
Post a Comment