KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), Elirehema Moses Kaaya, leo Agosti 11, 2020 amefanya ziara katika Haspitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime na kituo cha afya Magena ambapo ameeleza kuridhishwa na miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa nyumba tatu za watumishi unaogharimu Sh milioni 167, jengo la wagonjwa wanaosubiri huduma na duka la dawa katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Kaaya amesema Kituo cha Afya Magena ni miongoni mwa vituo 352 vilivyojengwa chini ya uongozi wa Rais Dkt John Pombe Magufuli.
Ujenzi wa kituo hicho chenye majengo mbalimbali yakiwamo ya wagojwa wa nje, mama na mtoto, maabara, wodi, upasuaji na kuhifadhi maiti, umegharimu Sh zaidi ya milioni 400.
Aidha, Kaaya ameipongeza Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa kutenga Sh zaidi ya milioni 60 kutoka mapato yake ya ndani kugharimia ujenzi wa uzio na mfumo wa umeme kituoni hapo.
Katibu Mkuu wa ALAT, Elirehema Moses Kaaya (kulia) akikagua duka la dawa la Hospitali ya Mji wa Tarime, leo. |
Halmashsuri hiyo inakabiliwa na ukosefu wa maji, lakini Kaaya amepongeza Mkurugenzi na watendaji wake kwa kusimamia matumizi mazuri ya fedha za halmashauri, lakini pia kwa ubunifu wao wa kuweka mikingio ya maji na matanki zaidi ya matano yenye ujazo wa lita 5,000 kila moja.
“Upatikanaji wa mashine za kieletroniki kukusanyia mapato umesaidia kuongeza ufanisi wa kazi kwani kwa kutumia mashine hizo hakuna udanganyifu kuhujumu mapato,” amesema Kaaya.
Katibu Mkuu wa ALAT, Elirehema Moses Kaaya (kulia) akiteta jambo na Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mji wa Tarime, Dkt Innocent Kweka, leo. |
Katibu Mkuu huyo wa ALAT, ametumia nafasi hiyo pia kutoa mwito kwa halmashauri zote nchini kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha za serikali ili kuchochoa maendeleo ya wananchi.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Dkt Innocent Kweka, amesema ukamilikaji wa miradi ya afya utasaidia wafanyakazi kuwa karibu zaidi na wagonjwa ili kutoa huduma kirahisi na kwa wakati.
Nao baadhi ya wakazi wa mtaa wa Magena, John Juma na Regina Michael, wameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuboresha na kuwasogezea karibu huduma za afya.
(Imeandikwa na Lilian Tesha, Tarime)
No comments:
Post a Comment