NEWS

Wednesday 5 August 2020

Saratani ya shingo ya kizazi hatari kwa wanawake

MIONGONI mwa saratani zinazoongoza kwa kuwasumbua wanawake ni saratani ya shingo ya kizazi inayotajwa iliongoza kwa asilimia 47 nchini mwaka 2019.

Haya yamesemwa na Meneja Kitengo cha Uchunguzi wa Saratani na Elimu kwa Umma kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dkt Maguha Stephano, wakati akionzungumza na waandishi wa habari waliotembelea banda lao katika viwanja vya Nyakabindi wilayani Bariadi, Simiyu ambapo maonesho ya Nanenane yanafanyika kitaifa kwa miaka mitatu mfululizo.

"Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na Taasisi ya Ocean Road kwa mwaka 2019 kwa upande wa wanawake saratani ya kizazi inaongoza kwa asilimia 47, saratani ya matiti (16%), saratani ya utumbo mkubwa na mdogo (5.8%), saratani ya koo (5.3%) na saratani ya kichwa na shingo ni (4.2%)," amesema Dkt Maguha.

Kwa upande wa wanaume, Dkt Maguha amesema saratani inayoongoza ni tezi dume kwa asilimia 23, saratani ya koo la chakula (26%), saratani ya kichwa na shingo (12%), saratani ya utumbo mkubwa na mdogo (11.4%) na saratani ya matezi (9%).
Mteja (kulia) akipata huduma kwenye banda la Ocean Road katika maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Nyakabindi wilayani Bariadi, Simiyu

Dkt Maguha amesema katika maonesho hayo wanatoa huduma ya uchunguzi wa awali wa saratani, elimu na ushauri wa namna ya kujikinga na saratani, jinsi ya kuishi na saratani na elimu ya lishe bora ambavyo vinatolewa bure.

Amesema pia wanatoa huduma ya kupima homa ya ini na chanjo ili kuepuka saratani ya ini huku na kwamba wanao wataalamu wa kutosha kwenye maeneno ya maonesho ya Nanenane.

Amewaomba wananchi kuzingatia mazoezi ili kupunguza unene uliokithiri, kula mboga mboga na matunda kwa wingi, kuepuka matumizi ya tumbaku, kuepuka au kupunguza matumizi ya pombe kupita kiasi, kuwa na utaratibu wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara.

Dkt Maguha pia ameshauri mabinti wenye umri wa miaka tisa hadi 14 kupata chanjo dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi na wenye ulemavu wa ngozi kuzingatia uvaaji wa nguo zinazofunika mwili, kofia na kutumia mafuta na losheni maalumu kwa ajili yao.

Katika hatua nyingine, amewaomba wananchi hususan kutoka maeneo na mikoa ya karibu na Simiyu kujitokeza kwa wingi kwenye banda la Ocean Road ambapo huduma zimesogezwa karibu kwani kuwahi mapema kunamsaidia mgonjwa kupata matibabu yatakayomwezesha kupona tofauti na yule anayechelewa na kusababisha saratani kusambaa.

Anna Naftari ni miongoni mwa wananchi waliofika kwenye banda la Ocean Road Nyakabindi, amesema huduma zinazotolewa hapo ikiwemo elimu na ushauri zitawasaidia wengi hususan watakaofika kwenye banda hilo kujua afya zao mapema na kama watakutwa wapo salama wajue namna ya kujikinga na wakikutwa tayari wana saratani wapate matibabu sahihi na kwa wakati.

(Imeandikwa na Anita Balingilaki, Bariadi)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages