NEWS

Thursday 13 August 2020

World Vision yaisaidia Sekondari ya Simiyu vitanda, magodoro

Kaimu Meneja wa Klasta ya Nzega, Gilselda Balyagati (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga (kulia) wakati wa makabidhiano ya msaada wa magodoro
 

SHIRIKA lisilo la kiserikali linalojishughulisha na maendeleo, misaada wakati wa majanga na utetezi (World Vision Tanzania) limekabidhi msaada wa vitanda 50 (double decker) na magodoro 100 katika Shule ya Sekondari ya Simiyu, vyote vyenye thamani ya shilingi milioni 26.6.

 

Akikabidhi msaada huo, Kaimu Meneja wa Klasta ya Nzega, Gilselda Balyagati, alisema shirika hilo limeamua kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuhakikisha watoto wanapata elimu bora ngazi ya msingi na sekondari.

 

Balyagati amesema kupitia mradi wa Kanadi shirika hilo limeweza kupata fedha kiasi za kusaidiaununuzi wa vitanda na magodoro kwa wanafunzi wa bweni, hasa wasichana ili kuwawezesha kusoma katika mazingira bora.

 

Ameongeza kuwa lengo la kutoa msaada huo ni kuchangia na kusaidia juhudi za kuwalinda wasichana dhidi ya vishawishi na mapambano dhidi ya ndoa na mimba za utotoni, ambapo katika mkoa wa Simiyu shirika hilo lina miradi mitano katika sekta za afya na maji.

 

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka  mara baada ya kupokea msaada huo na kuukabidhi kwenye uongozi wa shule hiyo jana, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga, amewataka wanafunzi kuyatunza vizuri na kusisitiza kuwa magodoro hayo yasiwafanye wapende usingizi na kuacha kujisomea.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga akiangalia magodoro yaliyotolewa msaada na World Vision Tanzania
 

Awali, Afisa Tawala Mkoa wa Simiyu, Ernest Hinju, amesema kwamba kupitia juhudi serikali ya mkoa na wadau, watoto wameweza kukaa kambi,hivyo kupata muda wa kutosha kujisomea na kusaidia kupunguza daraja sifuri kwenye matokeo ya kidato cha nne mwaka 2019 na hatimaye  kwenye mtihani wa taifa na kufanikiwa kuingia nafasi tano bora kitaifa.

 

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Simiyu, Mwalimu Vestina Sedekia, amelishukuru shirika hilo kwa kutoa msaada huo akisema wamewasaidia wanafunzi, hususan wasiokuwa na uwezo.

 

"Msaada huu ni wa muhimu, unakuta familia ina godoro moja la kulalia watoto hata wanne, hivyo inakuwa vigumu mtoto anayetaka kwenda bweni (kambi) kubeba lile godoro na awaache wenzake hawana la kulalia, hivyo msaada huo ni wa muhimu,” amesema Mwalimu Sedekia.

Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Simiyu siku ya kupokea msaada wa vitanda na magodoro kutoka World Vision Tanzania
 

Kwa upande wao, wanafunzi wa shule hiyo akiwemo Kwiyeya Buluba na Rita Masunga wamelishukuru shirika hilo kwa kutoa msaada huo huku wakikiri kuwa kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wanafunzi kuharibu magodoro na kuahidi kuwa watakuwa walinzi kwa wanafunzi ambao wamekuwa na tabia ya kufanya uharibifu ili waweze kuyatumia wao na wadogo zao wajao shuleni hapo.

 

{Imeandikwa na Anita Balingilaki, Bariadi)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages