
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, akizungumza na wakulima wa tumbaku katika mkutano uliofanyika Jumanne Julai 21, 2026 katani Mbogi.
Tarime
------------
Wakulima wa tumbaku waliokopa pembejeo kupitia Vyama vya Msingi vya Ushirika na Masoko (AMCOS) wilayani Tarime, Mara wametakiwa kulipa mikopo hiyo ili kuwezesha usambazaji wa pembejeo katika msimu ujao wa 2026/2027.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, alitoa maelekezo hayo Jumanne Julai 21, 2026, katika mkutano na wakulima wa zao hilo uliofanyika kata ya Mbogi.

Sehemu ya wakulima hao wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi katika mkutano huo.
"Uaminifu ndio mtaji, watu waliingia mikataba, tumejiridhisha tumbaku ilikuwepo ikavunwa ikapelekwa kwa nchi ambayo haikuwapa dhamana ya ruzuku, ardhi yetu, wataalamu wetu, tumbaku mkapeleka nchi nyingine.
"Maafisa kilimo walipita, mlikuwa na mazao ya tumbaku, baada ya kuvuna mkatorosha kwenda Kenya, ile fedha ni ya umma lazima zirudi kupitia AMCOS,” alisema Meja Gowele na kuendelea:
"Naagiza OCD, WAMACU andaa mashitaka kila mmoja awajibike kwa kile alichokopa, hatuwezi kuua kilimo cha tumbaku kwa sababu ya watu wachache, kuna wengine walichukua pembejeo ya mkopo hawana shamba wakaenda kuuza.”
Aidha, Meja Gowele aliwataka wakulima kuwa wazalendo kwa kuacha kutorosha wa zao la tumbaku kwenda nje ya nchi kwani kufanya hivyo kunaikosesha serikali mapato ambayo hutumika kutekeleza huduma na miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Awali, Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara (WAMACU Ltd), Samwel Gisiboye, alitaja AMCOS zinazodaiwa kuwa ni Nyakonga, Itiryo, Sirari, Mwesu, Kubiterere na Mbogi, akibainisha kuwa wakulima hao wanadaiwa mikopo pembejeo zenye thamani ya shilingi milioni 386.458.

Meneja Mkuu wa WAMACU Ltd, Samwel Gisiboye, akizungumza katika mkutano huo. (Picha zote na Mara Online News)
"Kama walipata masoko mazuri wakauza mitumba yao ya tumbaku, walipe mikopo ili tuweze kuagiza mbolea na mahitaji mengine wakulima waweze kwenda shambani msimu ujao,” alisema Gisiboye.
Nao wakulima wa tumbaku waliokwishalipa mikopo yao waliiomba serikali kuwachukulia hatua wote ambao walipewa mikopo ya pembejeo wawajibike kuilipa ili kuwezesha usambazaji wa huduma ya pembejeo katika msimu ujao.
"Tunaodaiwa tukamatiwe tulipe maana wengine walikuwa wanachukua pembejeo na wanaenda kuuza,” alisema mmoja wa wakulima hao.
No comments:
Post a Comment