NEWS

Tuesday 18 August 2020

Naibu Waziri Aweso aridhishwa ujenzi tenki la maji Musoma

Naibu Waziri Juma Aweso akitoa maelekezo katika eneo la mradi huo.
 

NAIBU Waziri wa Maji, Juma Aweso, jana Agosti 17, 2020 amekagua maendeleo ya ujenzi wa tenki la maji linalolenga kupanua mtandao wa huduma ya maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria, inayotolewa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA).

 

Aweso ameeleza kuridhishwa na kazi inayofanywa na kampuni ya JANDU inayojenga tanki hilo litakalokuwa na ujazo wa lita milioni tatu. Ujenzi wa tenki hilo umefikia asilimia 65 kwa sasa.

 

Mkurugenzi wa MUWASA, CPA Joyce Msiru, amemweleza Naibu Waziri Awezo kuwa mradi huo ukikamilika utaifanya mamlaka hiyo kupanua huduma ya maji kwa wakazi wa Manispaa wa Musoma wakiwemo wananchi wanaoishi pembezoni na vijiji jirani katika wilaya ya Butiama.

Naibu Waziri wa Maji, Juma Aweso (mwenye koti jeusi), akikagua ujenzi wa tenki la maji litakalokuwa na ujazo wa lita milioni tatu kwa ajili ya kusambaza maji kwa wakazi wengi zaidi wa Manispaa ya Musoma. Anayetoa maelezo ya mradi kwa Naibu Waziri huyo ni Mkurugenzi wa MUWASA, CPA Joyce Msiru.

Licha ya vijiji vya pembezoni, ujenzi wa tenki hilo, kwa mujibu wa CPA Msiru, utaiwezesha MUWASA kufikia maeneo yenye miinuko katika kata za Bweri, Makoko, Buhare na Kwangwa.

 

Hadi sasa asilimia 95 ya wananchi wa Manispaa wa Musoma wamefikiwa na huduma ya maji inayotolewa na MUWASA, hivyo kufikia lengo la ilani ya uchaguzi wa mwaka 2015, kwa mujibu wa CPA Msiru.

 

Naibu Waziri Awezo ameitaka mamlaka hiyo kuendelea kuwaunganishia wananchi huduma ya maji ya bomba kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

 

(Imeandikwa na Lubango Mleka, Musoma)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages