Katibu wa Hamasa na Chipukizi wa UVCCM Wilaya ya Serengeti, Chief Mosabi. |
KATIBU wa Hamasa na Chipukizi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Chief Mosabi, amesema wagombea wa chama hicho nafasi za urais, ubunge na udiwani watapata ushindi wa kishindo wilayani humo.
Mosabi ameyasema hayo katika mahojiano maalumu na Mara Online News leo asubuhi ambapo amemtabiria mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Dkt John Magufuli ushindi kwa asilimia 97.9, mgombea ubunge jimbo la Serengeti, Amsabi Jeremiah (asilimia 95) na madiwani wa chama hicho wilayani humo (asilimia 96).
Tathmini hiyo ya Mosabi chini ya Mwenyekiti wake, Bernard Nyaitamboka, imetokana na mwitikio mkubwa wa wananchi kwa wagombea wa CCM kwenye mikutano ya kampeni za Uchaguzi Mkuu utakaofanyika kesho Jumatano Oktoba 28, 2020.
"Lakini pia ikumbukwe kwamba jimbo al Serengeti linaundwa na kata 30, kati ya hizo, tayari kata 15 wagombea wetu wa CCM wamepita bila kupingwa, na tuna uhakika kuwa kata 15 zinazoingia kwenye uchaguzi wagombea wetu wote watashinda kwa kishindo," ameongeza katibu huyo wa hamasa na chipukizi wa UVCCM Wilaya ya Serengeti.
"Sisi wana-Serengeti hatudanganwi, tunaye Dkt Amsabi Jeremiah mwenye uwezo wa kutuletea maendeleo na kuendeleza mambo mazuri yaliyoachwa na mheshimiwa Marwa Ryoba, lakini pia kutokana na maendeleo makubwa ambayo mheshimiwa Rais Magufuli ametuletea nchini, tunamwongezea miaka mitano ili aendelee kutuletea maendeleo makubwa zaidi," amesema Mosabi.
(Imeandikwa na Mara Online News)
No comments:
Post a Comment