NEWS

Monday 26 October 2020

Watu 14 kizimbani kwa uvunjifu amani Simiyu

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, ACP Richard Abwao, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)  ofisini kwake jana

 

JESHI la Polisi mkoani Simiyu limewafikisha mahakama watu 14 kwa makosa tofauti yakiwamo ya uvunjifu wa amani.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, ACP Richard Abwao, amewambia waandishi wa habari jana kwamba washitakiwa hao wanatuhumiwa kutenda makosa hayo katika tarafa za Dutwa, Nkololo wilayani Bariadi na kata ya Kisesa wilayani Meatu.

 

ACP Abwao amefafanua kuwa uhalifu huo ulihusisha kumfanyia fujo mgombea udiwani, Ng'wani Edward, akiwataja watuhumiwa wa tukio hilo kuwa ni Kinyambo Tela na Maguha Lukonge wanaodaiwa kumrushia mawe nyumbani kwake.

 

Aidha, amesema Manamba Matondo alikutwa ndani ya nyumba ya mgombea udiwani, Emmanuel Makali, akiwa anafanya vitendo vya kishirikina kwa kumwaga dawa za kienyeji sakafuni.

 

Kwa upande mwingine, Kamanda Abwao amesema wakazi wa kijiji cha Gasuma, Budaga Butwage, Mbuta Maduhu na Saku Maduhu ambao pia ni wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walijeruhiwa na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kwamba watuhumiwa wanne wa tukio hilo walikamatwa. 

Katika hatua nyingine, Kamanda huyo amesema nyumba ya Manoni Malimi ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vjana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Kijiji Nkindwabiye ilibomolewa na wafuasi wa Chadema baada ya kuwazuia kufanya mkutano nyumbani kwake na kwamba Huma Lukanze amefikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.

 

Kamanda Abwao ameongeza kuwa Oktoba 24, 2020 jioni, Peter Paulo na wenzake watano waliingia kwenye ofisi ya kijiji cha Mwakaluba na kuchukua nyaraka mbalimbali, kisha kumshambulia mwenyekiti wa kijiji hicho, Kasuka Samba.

 

(Imeandikwa na Anita Balingilaki, Simiyu)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages