NEWS

Thursday 15 October 2020

IGP Sirro awaondoa hofu wananchi Tarime

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro (kulia) akipokea salamu kutoka kwa askari wa kikosi cha FFU TarimeRorya alipowasili mjini Tarime kabla ya kuanza kikao na wagombea ubunge na voiongozi wa vyama vya siasa leo. Kushoto ni RPC Mkoa wa Kipolisi TarimeRorya, William Mkonda. (Na Mpigapicha Wetu)


MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro amewaondoa hofu wakazi wa majimbo ya Tarime Mjini na Vijijini akisema jeshi hilo limejipanga kikamilifu kuhakikisha vitendo vya vurugu havitokei na kuathiri uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

 

“Suala la kwamba kutakuwa na vurugu niwahakikishie wana-Tarime kuwa hilo halitakuwepo, uwezekano huo haupo, uwezekano kwamba mtu atatangazwa kuwa ameshinda wakati hakushinda haupo, huo uwezo kwanza ataupata wapi, hiyo nguvu ataitoa wapi,” amesema IGP Sirro.

 

Amesisitiza hayo mjini Tarime leo mchana katika kikao maalumu na viongozi wa vyama vya siasa na wagombea ubunge kutoka majimbo ya Tarime Mjini, Tarime Vijijini na Rorya mkoani Mara.

Mgombea ubunge jimbo la Tarime Vijijini kwa tiketi ya CCM, Mwita Waitara akizungumza katika kikao hicho.

 

IGP Sirro ametumia kikao hicho kuwasihi wanasiasa wa maeneo hayo kuacha kasumba ya fujo na kutoruhusu suala la uchaguzi kuwagawa wananchi na kutowesha amani katika jamii.

 

“We have to change (tunapaswa kubadilika), sisi sote ni ndugu, kwanini tuumizane kwa kitu [akimaanisha uchaguzi] kinachopita. Kwanini uwaandae vijana kuingia barabarani kufanya vurugu, mbona huwambii watoto wako waingie barabarani?

 

“Tuzungumze sera, habari ya vurugu haitalipa… wanasiasa pendaneni, hii habari ya kupigana ni ushamba tu,” amesema mkuu huyo wa jeshi la polisi.

Mgombea ubunge jimbo la Tarime Mjini kupitia NCCR Mageuzi, Mary Nyagabona akizungumza katika kikao hicho.

Katika kikao hicho, IGP Sirro amewapa wagombea ubunge na viongozi wa vyama vya siasa nafasi ya kueleza changamoto zao ambapo baadhi wametuhumiana kufanyiana vurugu na wengine wamelalamika kuonewa na jeshi la polisi.

Mgombea ubunge jimbo la Rorya kwa tiketi ya CCM, Jafari Chege akitoa ushauri katika kikao hicho.

 

Hata hivyo, IGP Sirro amewaomba wanasiasa hao kusahau yaliyopita, badala yake wafungue ukurasa mpya na kuelekeza nguvu zaidi kwenye sera za kushawishi wananchi kuwachagua.

Mgombea ubunge jimbo la Tarime Mjini kwa tiketi ya Chadema, Esther Matiko akizungumza katika kikao hicho.

 

Miongoni mwa wagombea ubunge waliohudhuria kikao hicho, majimbo na vyama vyao vikiwa kwenye mabano ni Esther Matiko (Tarime Mjini - Chadema), Michael Kembaki (Tarime Mjini – CCM), Mwita Waitara (Tarime Vijijini – CCM), Mary Nyagabona (Tarime Mjini – NCC Mageuzi), Jafari Chege (Rorya – CCM), John Heche (Tarime Vijijini – Chadema) na Charles Mwera (Tarime Vijijini – ACT Wazalendo).

Mgombea ubunge jimbo la Tarime Vijijini kupitia ACT Wazalendo, Charles Mwera akijenga hoja katika kikao hicho.
  

Mgombea ubunge jimbo la Tarime Vijijini, John Heche (Chadema) akiongea katika kikao hicho.

 

(Imeandikwa na Christopher Gamaina, Tarime)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages