NEWS

Tuesday 13 October 2020

Kembaki aomba jembe la maendeleo Tarime Mjini

Mgombea ubunge jimbo la Tarime Mjini kwa tiketi ya CCM, Michael Kembaki akiomba kura kwa wakazi wa kata ya Nyamisangura (hawapo pichani) jimboni humo, jana.


MGOMBEA ubunge Tarime Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Michael Kembaki amesema endapo atachaguliwa Oktoba 28, mwaka huu atakuwa amekabidhiwa jembe la maendeleo ya jimbo hilo.

 

Kembaki ametoa kauli hiyo ya kufananisha ubunge na jembe la maendeleo wakati akiomba kura kwa wananchi kwenye mkutano wake wa kampeni uliofanyika katika kata ya Nyamisangura jimboni humo, jana.

 

“Nawaombeni ridhaa yenu tushirikiane kuleta maendeleo ya kata hii [Nyamisangura] na jimbo la Tarime Mjini kwa ujumla… nipeni jembe [akimaanisha kura za ubunge] nikalime maendeleo,” Kembaki amewaomba wakazi wa kata hiyo.

 

“Nina hofu ya Mungu, nipeni jembe la maendeleo. Mwaka 2015 sikuchaguliwa lakini kila nilichokipata nimekuwa nikijinyima kwenda kufanya starehe Dubai [nchi ya Falme za Kiarabu] kama mtani wangu wa jadi (hakumtaja), ila nimekuwa nikikileta jimboni hapa kukitumia na wenzangu kutatua changamoto zinazotukabili,” amesema.

Michael Kembaki (juu kushoto) akiomba kura za ubunge wakazi wa kata ya Nyamisangura, jana. (Picha zote na Peter Hezron)

 

Mgombea ubunge huyo amesema bado kata ya Nyamisangura na jimbo la Tarime kwa ujumla kuna changamoto katika sekta za maji, barabara, afya, elimu na umeme zinazohitaji kutatuliwa ili wananchi wapige hatua ya maendeleo ya kiuchumi na kimaisha.

 

Huku akizungumza kwa kujiamini zaidi, Kembaki amesisitiza ahadi za kuleta maendeleo ya kisekta na kuboresha maslahi ya makundi yote ya jamii wakiwamo wazee, vijana, wanawake, wajasiriamali na wafanyabiashara.

Mgombea ubunge jimbo la Tarime Mjini kupitia CCM, Michael Kembaki kwenye mkutano wake wa kampeni uliofanyika katika kata ya Nyamisangura, jana.

 

“Kwa hiyo ndugu zangu mimi ni kijana wenu, ninawaomba kura za Rais Dkt John Magufuli aongeze kasi ya maendeleo kwa miaka mitano mingine ijayo, nipigieni kura niwe mbunge wenu na mpigieni kura mgombea mwenzetu wa CCM awe diwani wa Nyamisangura tushirikiane kuleta maendeleo ya kweli katika jimbo letu la Tarime Mjini,” amesisitiza Kembaki.

 

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages