NEWS

Sunday 8 November 2020

RC Malima aeleza Mara ilivyo kinara kwa fursa za kiuchumi

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima.

 

MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Adam Malima, ameainisha jinsi mkoa huo ulivyo na fursa za kipekee ambazo zikutumiwa vizuri zitaufanya kuongoza kwa maendeleo ya kiuchumi nchini.

 

“Mkoa wa Mara ni tajiri, una fursa nyingi kuliko mikoa mingine Tanzania,” Malima ameyasema hayo alipokutana na viongozi wa dini ambao ni wajumbe wa kamati ya amani ya mkoa huo mjini Musoma hivi karibuni, kujadili umuhimu wa kutunza amani.

 

RC Malima amesema mkoa huo umejaaliwa kuwa na sehemu kubwa ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA)) inayopokea maelfu ya watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani.

 

“Mungu akupeni nini! Mkoa wa Mara ndio wenye mbuga ya Serengeti ambayo ni kivutio bora cha utalii barani Afrika,” amesisitiza.

Watalii wakifurahia kutazama na kupiga picha makundi ya nyumbu katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

 

Amesema uwekezaji mkubwa wa kuboresha na kupanua uwanja wa ndege wa Musoma utaufanya mkoa wa Mara kuwa lango kuu la watalii wanaoingia nchini kwa ajili ya kutembelea hifadhi hiyo yenye hadhi ya maajabu saba ya urithi wa dunia.

 

Malima amesema mkoa huo pia una utajiri mkubwa wa madini akitolea mfano mgodi wa dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime.

 

“Mikoa ya Mara na Geita ndio inaongoza kwa kuwa na dhahabu nyingi nchini,” amesema mkuu huyo wa mkoa.

Dhahabu

 

Aidha, amezungumzia kilimo cha zao la kahawa aina ya Arabika akisema nacho ni fursa ya kiuchumi ya kipekee iliyopo mkoani humo. “Imethibitika kuwa kahawa ya Arabaka inayozalishwa Mara ni bora,” amesema.

 

Kahawa hiyo inayozalishwa kwa wingi wilayani Tarime, ina soko kubwa katika mataifa mbalimbali yakiwamo ya Ulaya.


Kahawa

Malima ametaja pia Ziwa Victoria kuwa ni fursa nyingine kubwa ya kiuchumi mkoani Mara. “Mkoa wa Mara ndio una mazalia makubwa ya samaki, na pamba bora inalimwa mkoani hapa,” ameongeza.

Ziwa Victoria


 

Sato ni mojawapo ya aina za samaki wanaopatikana katika Ziwa Victoria.

Amesema kinachotakiwa ni kutumia fursa hizo vizuri kwa ajili ya maendeleo ya mkoa huo na taifa kwa ujumla.

 

Mbali na amani, RC Malima amewaomba viongozi wa dini kuwa sehemu ya kupaisha maendeleo ya mkoa huo.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, akichapa kazi ofisini kwake.

 

Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mara, Msabaha Kassim, amemwelezea mkuu huyo wa mkoa kama kiongozi makini mwenye maono ya kuleta mapinduzi makubwa ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

 

“Namshukuru Mheshimiwa Rais Dkt John Magufuli kwa kutuletea mkuu wa mkoa makini,” amesema kiongozi huyo wa kiroho.

 

(Imeandikwa na Mara Online News)

 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages