NEWS

Friday 10 September 2021

DC Serengeti ataka kila mfanyabiashara kulipa kodi




MKUU wa Wilaya (DC) ya Serengeti, Dkt Vicent Mashinji (pichani juu) amehimiza wafanyabiashara wote wilayani humo wakiwemo wa vijijini kulipa kodi.

“Nawaomba waandishi wa habari, sambazeni taarifa hizi ili wananchi waelewe kuwa ni wajibu wa kila mwananchi ambaye ni mfanyabiashara kulipa kodi kwa wakati hata kama biashara yake ipo kijijini,” Dkt Mashinji amesema katika kikao na waandishi wa habari jana ofisini kwake, jana Ijumaa.

Amesema ukusanyaji wa mapato ni muhimu kwa maendeleo ya taifa, lakini pia unaiwezesha halmashauri ya wilaya hiyo kutekeleza miradi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Mfano, Dkt Mashinji amesema mji wa Mugumu ambao ni makao makuu ya wilaya hiyo, unapaswa kuendelezwa kuwa wa kisasa ili kuendana na hadhi ya wilaya hiyo ambayo eneo lake kubwa ni Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

“Mji wetu ni wa kitalii, lazima ukuwe na zaidi ya yote, halmashauri inayokusanya mapato ndiyo inayopata maendeleo zaidi,” DC Mashinji amesema na kusisitiza kuwa kila mfanyabiashara lazima alipe kodi bila kuonewa.

Amesema elimu zaidi kwa wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kulipa kodi itaendelea kutolewa katika wilaya hiyo na kuonya kuwa watakaokaidi, au kufanya udanganyifu wa kutolipa kodi watakiona cha moto.

“Ukusanyaji wa kodi hakuna huyu ni maarufu na ukaguzi ukifanyika ukakutwa haulipi kodi hakuna msamaha,” amesisitiza.

Amesema atakuwa anapita kila eneo la wilaya hiyo kuhakikisha ukusanyaji wa mapato unasimamiwa vizuri.

DC Mashinji alitumia nafasi hiyo pia kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayofanya kuhakikisha ukusanyaji wa kodi unaenda vizuri na kuiwezesha Serikali kugharimira miradi mikubwa ya maendeleo nchini.

Mkuu huyo wa wilaya amehimiza pia matumizi ya mashine za EFD bila kufanya udanganyifu.

Ametoa wito pia kwa madereva wa pikipiki za abiria (bodaboda) kukata leseni kwa ajili ya kuendesha shughuli zao.

(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages