NEWS

Sunday 12 September 2021

Rais Samia afanya uteuzi wa mawaziri, Kalemani, Ndugulile ‘out’, Makamba, Mbarawa waula




RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (pichani juu) amefanya uteuzi wa nafasi za uongozi serikalini, ukiwemo wa mawaziri watatu.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais - Ikulu, Jafafar Haniu kwa vyombo vya habari jana Septemba 12, 2021, inasema Rais Samia amemteua Dkt Stergomena Lawrence Tax kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Elias John Kwandikwa aliyefariki dunia hivi karibuni.

Pia Rais amemteua Dkt Ashatu Kachwamba Kijaji kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Dkt Faustine Ndugulile ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

“Aidha, Mheshimiwa Rais ameihamishia Idara ya Habari katika Wizara hii [Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari] kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,” taarifa hiyo imesema.

Rais Samia pia amemteua January Yusuf Makamba kuwa Waziri wa Nishati, akichukua nafasi ya Dkt Merdard Kalemani ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Mwingine ni Profesa Makame Mnyaa Mbarawa aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, akichukua nafasi ya Dkt Leonard Madaraka Chamuriho ambaye pia Rais ametengua uteuzi wake.

Wakati huo huo, Rais Samia amemteua Dkt Eliezer Mbuki Feleshi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akichukua nafasi ya Profesa Adelardus Kilangi ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mawaziri Wateule hao na Mwanasheria Mkuu huyo wa Serikali wataapishwa leo Septemba 13, 2021 saa 5:00 asubuhi Ikulu, Chamwino jijini Dodoma.

#MaraOnlineNews-Updates

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages