NEWS

Friday 19 April 2024

Mfahamu kwa kina Mkuu wa Majeshi wa Kenya Jenerali Ogolla aliyekufa katika ajali ya helikopta



Jenerali Francis Omondi Ogolla enzi ya uhai
------------------------------------------------

KIFO cha Mkuu wa Majeshi (CDF) ya Kenya, Jenerali Francis Omondi Ogolla kimeishtua nchi baada ya Rais William Ruto kutangaza habari hizo za kusikitisha.

Jenerali Ogolla alithibitishwa kufariki katika ajali ya helikopta eneo la Kaben, Marakwet Mashariki jana Alhamisi.

Jenerali Ogolla aliteuliwa kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi katika mabadiliko ndani ya jeshi Aprili 2023. Alichukua nafasi hiyo kutoka kwa Jenerali Robert Kibochi ambaye alistaafu akiwa na umri wa miaka 62.

Kabla ya uteuzi huo, Jenerali Ogolla alikuwa Makamu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Kenya.

Taaluma ya jeshi
Aprili 28, 2023, Rais Ruto alimpandisha cheo Luteni Jenerali Francis Omondi Ogolla kuwa Jenerali na kumteua Mkuu wa Majeshi ya Kenya.

Jenerali Ogolla alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Kenya Aprili 24, 1984 na Mei 6, 1985 aliteuliwa kuwa Luteni wa Pili na kutumwa kwa Jeshi la Wanahewa la Kenya.

Alipata mafunzo ya urubani wa ndege na USAF na kama rubani mkufunzi katika Jeshi la Wanahewa la Kenya (KAF).

Pia alipata mafunzo katika nyanja zingine zikiwemo ujasusi wa picha, kukabiliana na ugaidi na uchunguzi wa ajali.

Jenerali Ogolla ni mhitimu wa ÉcoleMilitaire de Paris na Chuo cha Kitaifa cha Ulinzi cha Kenya.

Ana Diploma katika Masomo ya Kimataifa na Sayansi ya Kijeshi kutoka Chuo Kikuu cha Egerton, Shahada ya Sanaa katika Sayansi ya Siasa, Migogoro ya Silaha na Mafunzo ya Amani (Heshima za Daraja la Kwanza) na Shahada ya Uzamili ya Sanaa katika Mafunzo ya Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.

Alipanda vyeo hadi kuwa Meja Jenerali na kuteuliwa kuwa Kamanda wa Jeshi la Wanahewa la Kenya Julai 15, 2018 wadhifa ambao aliutumikia kwa miaka mitatu.

Aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali katika mafunzo, kamandi na wafanyakazi, ikiwa ni pamoja na Naibu Kamanda wa Jeshi la Anga la Kenya, Kamanda wa Kambi ya Laikipia Air Base, Afisa Mkuu wa Kitengo cha Tactical Fighter Wing, Mkufunzi Mkuu wa Usafiri wa Ndege katika Shule ya Mafunzo ya Anga kwa Jeshi la Anga la Kenya na Afisa wa Dawati la Operesheni katika Jeshi la Wanahewa la Kenya.

Pia, alihudumu katika iliyokuwa Yugoslavia kama Mwangalizi na Afisa Habari wa Kijeshi kutoka mwaka 1992 hadi 1993, kama Mwenyekiti wa Ushirika wa Kijeshi wa Kikristo kutoka mwaka 1994 hadi 2004 na Mwenyekiti mwenza wa Chama cha Wakuu wa Wanajeshi wa Angani wa Afrika kati ya mwaka 2018 na 2019.

Alikuwa na mke aitwaye Aileen, na amebarikiwa kuwa na watoto wawili na mjukuu. Alikuwa akipenda kusoma na kucheza gofu.



CDF au Mkuu wa Majeshi ndiye afisa wa ngazi ya juu zaidi wa kijeshi katika Jeshi la Ulinzi la Kenya na mshauri mkuu wa kijeshi wa Rais wa Kenya na Baraza la Usalama la Kitaifa.

Rais Ruto alieleza sababu za kumteua Ogolla kama Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) akisema: "Katika kuzingatia uteuzi wako, nilitathmini historia yako, ulikotoka, umefanya nini, na safari yako ya kijeshi, na nimeridhika kwamba unastahili."

"Wito wangu wa wazi ni wa kikosi kimoja, dhamira moja. Tutakuwa kikosi kimoja kilichounganishwa kwa lengo moja la kutoa ulinzi na kubaki waaminifu kwa kaulimbiu yetu ya Ulinzi Daima," alisema Jenerali Ogolla wakati akiapishwa.

Chanzo: BBC

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages