Kahawa ni miongoni mwa mazao ya
biashara yanayolimwa mkoani Mara.
--------------------------------------------------
Na Christopher Gamaina
chrisgapressman@gmail.com
----------------------------------------
Uzalishaji wa mazao
Masoko ya mazao
Mwito kwa wakulima
Na Christopher Gamaina
chrisgapressman@gmail.com
----------------------------------------
Mkoa wa Mara umebarikiwa kuwa na fursa za kilimo zinazoweza kutoa mchango mkubwa kwa ukuaji wa uchumi wa wakulima na taifa kwa ujumla.
Kahawa na tumbaku ni miongoni mwa mazao muhimu yanayostawi katika ardhi ya mkoa huu - kama hakuna changamoto za kiuchumi na uendeshaji zinazoweza kuathiri uzalishaji na maendeleo ya wakulima.
Wakulima wa mazao haya mkoani Mara wana kila sababu ya kujivunia uwepo wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima Mkoa wa Mara (WAMACU Ltd), ambacho kinaendelea kuweka mipango na mikakati madhubuti ya kusaidia wakulima kuongeza uzalishaji na kuboresha hali zao za kiuchumi.
Uzalishaji wa mazao
Tunashuhudia juhudi kubwa zinazofanywa na WAMACU, zikiwemo za elimu na mafunzo kwa wakulima kuhusu mbinu bora za kilimo na teknolojia mpya zinazoweza kuongeza uzalishaji wa kahawa na tumbaku, miongoni mwa mazao mengine ya biashara na chakula.
Kupitia mafunzo haya, wakulima wanapata uelewa kuhusu mbolea za kisasa, udhibiti wa magonjwa ya mazao, na mbinu bora za upandaji na uvunaji.
WAMACU inastahili pongezi kubwa kutokana na juhudi zake hizi kwa sababu kuwapa wakulima ujuzi ni hatua muhimu katika kuongeza tija na ubora wa mazao.
Vile vile, WAMACU ina fursa za upatikanaji wa pembejeo za kilimo, zikiwemo mboleza za ruzuku ya serikali kwa wakulima ili kuwawezesha kuimarisha shughuli za mashamba yao.
Kwa kutumia fursa hii, wakulima wanapata mahitaji yao ya kilimo kiurahisi na kwa gharama zilizo rafiki. Huduma zinazotolewa na WAMACU kwa wakulima zina masharti nafuu ikilinganishwa na kwingine.
Meneja Mkuu wa WAMACU Ltd,
Samwel Gisiboye.
--------------------------------------------
Masoko ya mazao
Moja ya changamoto kubwa ambazo zimekuwa zikiwakabili wakulima wa kahawa na tumbaku ni upatikanaji wa masoko ya uhakika. Lakini kwa sasa, WAMACU ina mikakati kabambe ya kupata masoko ya mazao hayo ndani na nje ya Tanzania, sambamba na kuboresha mnyororo wa usambazaji na uhusiano na wanunuzi.
Hatua hii inawezesha wakulima kupata bei nzuri za mazao yao na kuepuka upotevu wa mazao kwa sababu ya kukosa masoko ya uhakika.
Kwa upande wa msaada wa kitaalamu, WAMACU inashirikiana na maofisa ugani kutoka serikalini katika kuwapa wakulima mafunzo na ushauri wa kitaalamu kuhusu mbinu bora za kilimo chenye tija.
Kwa mfano, hivi karibuni WAMACU iliwezesha na kuratibu mafunzo ya mbinu bora za kilimo cha tumbaku kwa maofisa kilimo na watendaji wa Vyama vya Msingi vya Ushirika na Masoko (AMCOS) kutoka wilaya zinazolima zao hilo mkoani Mara.
Lakini pia, WAMACU Ltd inasaidia kupanga matumizi bora ya mbolea, teknolojia ya kisasa na kuboresha usimamizi wa shughuli za kilimo. Hatua hizi zinachangia kuongeza uzalishaji na kupunguza gharama za uzalishaji wa mazao.
WAMACU pia inaongeza juhudi za maendeleo ya kijamii kwa kuhamasisha umoja wa wakulima. Kupitia AMCOS, chama hiki kinasaidia wakulima kupata huduma nzuri, kubadilishana uzoefu, kufundishana na kushirikiana katika shughuli za kilimo.
Kutokana na uelewa wa kina kuhusu fursa hizi, ni muhimu kwa wakulima wa kahawa, tumbaku na mazao mengine mkoani Mara kuhakikisha wanatumia kikamilifu huduma zinazotolewa na WAMACU Ltd.
Kwa kushirikiana na chama hiki kikuu cha ushirika, wakulima wanaweza kupanua maeneo yao ya kilimo, kuboresha mbinu zao za kilimo, kuinua kipato chao cha fedha na hata mikopo, na kuongeza tija kwenye mazao wanayozalisha.
Kwa kufanya hivyo, ni dhahiri wakulima wa mkoani Mara watakuwa na uwezo wa kuongeza uzalishaji, kupunguza umaskini na kujiinua kiuchumi.
Hivyo, ni muhimu sana kwa wakulima wa kahawa, tumbaku na mazao mengine mkoani Mara kuhakikisha wanajiunga na WAMACU ili kuchangia katika juhudi za kuleta mapinduzi ya kilimo na maendeleo ya uchumi kwenye maeneo yao.
WAMACU Ltd imesimama imara kama mshirika na msaada wa maendeleo kilimo, hivyo ni muhimu kwa wakulima kutambua na kutumia fursa hii kwa manufaa yao na jamii nzima. Mkulima kukaa nje ya ushirika huu ni sawa na kuchagua kukosa huduma bora na nafuu za kilimo.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>> Kwanini uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura ni muhimu nchini
>>Taasisi ya Uhasibu Tanzania kuanzisha tawi lake Tanga
>>UWT CCM Mara wajivunia Mary Chatanda, sasa kuanzisha vitega uchumi vyao
>>HABARI PICHA:Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Dkt Samia Suluhu Hassan akikagua Gwaride Maalumu la Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam jana.
No comments:
Post a Comment