NEWS

Thursday, 12 September 2024

Rais Samia aahidi mema kwa vijana wanaohitimu elimu ya msingi



Rais Samia Suluhu Hassan

Na Mwandishi Wetu/ Mara Online News

Rais Samia Suluhu Hassan ameahidi kutoa nafasi kwa kila mwanafunzi atakayefaulu Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba na kujiunga na kidato cha kwanza mwaka ujao 2025.

Akitoa salamu za kuwatakia heri wanafunzi 1,230,780 wa darasa la saba nchini walioanza mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi jana, Rais alisema serikali yake imeandaa mazingira wezeshi kwa wanafunzi hao kujiandaa na safari nyingine ya kutoa mchango wao kwa maendeleo ya taifa.

Katika salamu hizo, Rais pia aliahidi azma ya serikali yake ya kuwasomesha wanafunzi hao bila kulipia ada kwa miaka minne ya sekondari, miaka miwili ya kidato cha tano na kidato cha sita na vyuo vya ufundi kwa kila wilaya kwa wanafunzi watakaochagua kujifunza fani hiyo.

Alieleza pia kwamba serikali itaendelea na utaratibu wake wa sasa wa kutoa mikopo kwa wanafunzi watakaofaulu mitihani ya kujiunga na vyuo vikuu nchini.

Rais Samia alisisitiza kwamba jitihada za kutoa elimu kwa vijana wa Tanzania zinakwenda sambamba na maboresho ya sera za kiuchumi ili ziweze kuzalisha fursa nyingi kwa kila mwanafunzi kadri anavyokua na kuingia katika kundi la nguvu kazi ya taifa.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages