Na Mwandishi Wetu/ Mara Online News


Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) Tanzania limefanya mkutano maalum na viongozi na watendaji wa mashirika yasiyo ya serikali yanayopambana na ukeketaji katika wilaya ya Tarime.
Mkutano huo ulifanyika mjini Tarime juzi, ambapo maafisa wa shirika hilo walijadiliana na wadau hao namna ya kuunganisha nguvu katika kupambana na ukatili huo wa kijinsia.
Pamoja na mambo mengine, walikubaliana kwamba elimu ndiyo yenye nafasi kubwa ya kubadilisha mitazamo ya jamii inayokumbatia mila ya ukeketaji kwa watoto wa kike.
“Elimu ikitolewa kwa ujumbe, njia na wakati sahihi itabadilisha imani za watu wanaoendekeza ukeketaji,” alisisitiza mwezeshaji kutoka WiLDAF Tanzania, Thomas Diwani Mponda.
Kabla ya mkutano huo, shirika hilo lilitumia siku mbili kuendesha mafunzo kwa walezi wa klabu za shule salama, sambamba na elimu ya ujasiriamali kwa wanawake.
Pia, lilitumia siku mbili nyingine kuendesha midahalo ya makundi mbalimbali ya jamii katika kata za Komaswa na Regicheri kuhusu namna ya kushirikiana katika mapambano dhidi ya ukeketaji.
Kwa mujibu wa Afisa Mradi wa WiLDAF Tanzania, Suzan Kawanga, shirika hilo linaendesha shughuli hizo katika wilaya za Tarime, Serengeti na Butiama mkoani Mara kupitia mradi wake wa Jamii Imara, chini ya ufadhili kutoka Ubalozi wa Marekani hapa nchini.
No comments:
Post a Comment