Na Mwandishi Wetu/ Mara Onine News,
Tarime
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Vijijini mkoani Mara umetoa sababu za kurejesha shilingi milioni 4.336 makao makuu ya mfuko huo.
Sababu mojawapo ni baada ya walengwa kutojitoleza kupokea fedha hizo za kusaidia kaya maskini.
Mratibu wa TASAF wa Halmashauri hiyo, Emmanuel Kadama aliiambia Mara Online News wilayani hapa juzi kwamba kwa kawaida fedha ambazo hazijachukuliwa na wahusika hurudishwa makao makuu ili kuunganishwa na malipo yanayofuata kwa ajili ya wahusika kuzichukua kwa pamoja.
Kadama alisema walengwa wanaoshindwa kuchukua malipo yao mara nyingi huwa wamesafiri bila kuacha watu mbadala wa kuwapokelea malipo.
Alisisitiza kwamba “malipo ya walengwa hawa hayachukuliwi na mtu mwingine yeyote hadi awe mhusika mwenyewe, au mwanakaya aliyekabidhiwa vielelezo vyote vinavyohitajika.”
Wiki iliyopita, madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime walieleza kutofurahishwa na taarifa ya kurudishwa shilingi milioni 4.336 makao makuu ya TASAF.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilianza kutekeleza mradi wa TASAF mwaka 2000, ikiwa ni moja ya mbinu za kuwezesha kaya masikini kuongeza vipato na fursa za kujikimu.
No comments:
Post a Comment