
Katibu Mkuu wa CCM,
Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi.
Chama tawala - CCM kimelaani utekaji na mauaji ya watu nchini kikisema tukio la hivi karibuni la mauaji ya kiongozi wa chama cha upinzani - CHADEMA, Ali Mohammed Kibao ni jambo la kusikitisha na kutia hofu kwa wananchi.
“Taifa linapita kwenye mtihani wa hofu miongoni mwa wananchi, na hatuwezi kulipuuza hilo… Mtu yeyote anayehatarisha usalama wa raia, mtu yeyote, ama kikundi kinachotekeleza matendo ya utekaji hawawezi kuwa na nia njema na CCM,” amesema Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi katika mkutano na wahariri waandamizi jijini Dar es Salaam leo.
Katibu Mkuu huyo wa chama tawala amesema kuwa matendo ya utekaji yanafanywa na watu wenye nia mbaya ya kufarakanisha taifa. “Jambo la utekaji na mauaji linatoa taswira mbaya kwa CCM. Hivyo hatuwezi kuunga mkono,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa matendo hayo yanafanya raia wasiwe na imani na polisi, na ameonya kwamba hilo likiendelea litaathiri usalama na ustawi wa nchi kwa ujumla.
“Ni muhimu sisi pamoja na wapinzani kushirikiana ili tusiwape genge la watekaji ushindi. Genge linataka kutufarakanisha,” amesema Dkt Nchimbi.
Kiongozi huyo amesema CCM inaunga mkono kauli ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kutaka uchunguzi ufanyike. “Niseme kuwa CCM imekerwa kweli kweli na jambo hili… Genge hili la watekaji linaweza kuwa popote, ndani ya CCM, polisi au hata CHADEMA. Muhimu ni kuacha uchunguzi wa kina ufanyike, na majibu yake yapatikane ili hatua zichukuliwe,” amesema.
Kuhusu hoja ya CHADEMA ya kutaka uchunguzi uongozwe na makachero kutoka mashirika ya kijasusi ya kimataifa kama Scotland Yard ya Uingereza, Dkt Nchimbi amesema CCM itaiunga mkono serikali kama itaona umuhimu wa kushirikisha mashirika ya kimataifa.
Hata hivyo, amesema misimamo ya CHADEMA ya kutaka Rais Samia ang’oke madarakani haiwezekani kwa kuwa yupo madarakani kikatiba na ataondoka pale tu muda wake wa kikatiba utakapoisha.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi nchini limepiga marufuku maandamano yaliyokuwa yamepangwa na CHADEMA kufanyika jijini Dar es Salaam Septemba 23, 2024.
Msemaji wa Jeshi hilo, David Misime ametoa onyo kwa viongozi wa chama hicho cha upinzani kuacha kuendelea kuwahamasisha wananchi kujihusisha na maandamano hayo.
“Jeshi la Polisi linatoa katazo kwa yeyote aliyealikwa, kuelekezwa kufika Dar es Salaam kutoka mkoa wowote ule kwa ajili ya maandamano hayo - asitubutu kufanya hivyo kwani maandamano hayo ni haramu na hayatafanyika,” amesema Misime.

Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania,
SACP David Misime.
Juzi Jumatano, Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, alisema nia ya maandamano hayo ni kudai uhai wa wanachama na viongozi mbalimbali wa chama hicho waliopotezwa.
Hata hivyo, SACP Misime ameonya kwamba waliopanga kuhudhuria wasipoteze muda na gharama zao kwani yeyote atakayeingia barabarani atakabiliwa vilivyo kwa mujibu wa sheria za nchi.
No comments:
Post a Comment