Katibu Tawala Mkoa wa Mara,
Gerald Musabila Kusaya.
------------------------------------
Na Mwandishi wa Mara Online News
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara imewaomba wakazi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utakaoanza kesho.
“Maandalizi yote yamekamilika na tayari vifaa vya kuandikishia vimeshasambazwa katika vituo vya kujiandikishia,” amesema Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Gerald Musabila Kusaya katika taarifa yake kwa vyombo vya habari leo.
Kusaya amefafanua kuwa shughuli hiyo itafanyika kuanzia kesho Septemba 4 hadi 10, 2024 na kwamba vituo vya kujiandikishia vitafunguliwa kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 12.00 jioni.
Amesema idadi ya vituo vitakavyohusika ni 1,597 katika mkoa mzima na majengo yatakayotumika ni ya umma ambayo yalitumika katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mwaka 2019/2020.
“Wahusika wa uboreshaji wa Daftari hilo ni mwananchi anayejiandikisha kwa mara ya kwanza ambaye ni raia wa Tanzania, mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea ambaye hakuwahi kujiandikisha kwenye Daftari, na atakayetimia miaka 18 ifikapo yatehe ya uchaguzi mkuu mwaka 2025.
“Mwananchi anayeboresha taarifa zake ni ambaye alijiandikisha awali na amehama eneo moja la uchaguzi kwenda linguine, ambaye taarifa zake zilikosewa wakati wa kujiandikisha na aliyepoteza, au kadi yake kuharibika.
“Hivyo, wananchi wa mkoani Mara tunawaomba mjitokeze kwa wingi ili muweze kuboresha taarifa zenu na kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Mpiga Kura ili kutimiza haki ya msingi ya kikatiba itakayowawezesha kushiriki katika uchaguzi,” amesema Kusaya.
Kaulimbiu ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura inasema: “Kujiandikisha kuwa Mpiga Kura ni Msingi wa Uchaguzi Bora.”
No comments:
Post a Comment