
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akihutubia mkutano wa hadhara jijini Dar es Salaam, leo Novemba 24, 2025..
Dar es Salaam
-------------------
Serikali imeagiza kufunguliwa kwa Kanisa la Ufufuo na Uzima, huku ikielekeza lipewe miezi sita ya uangalizi katika kuzingatia miiko, masharti na sheria za uendeshwaji wake.
Pia, serikali imeelekeza kurekebishwa kwa sharti linalotaka kufungiwa kwa nyumba ya ibada iwapo atakosea kiongozi, akisisitiza anayekosea ndiye aadhibiwe bila kuathiri waumini kufanya ibada.
Kanisa la Ufufua na Uzima lilifutiwa usajili Juni 2, 2025 baada ya kudaiwa kukiuka masharti ya uendeshaji wake - kwa kujihusisha na siasa.
“Natambua ilikuwepo hii moja ya Ufufuo na Uzima kaifungulie, ifungulie wape masharti ya uangalizi ndani ya miezi sita. Ziandikie taasisi zote za kidini kuzikumbusha miiko na mipaka ya ufanyaji kazi, sawa sawa na sheria na Katiba ya nchi yetu,” amesema Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba.
Waziri Mkuu Mwigulu ametoa maelekezo hayo leo Novemba 24, 2025 alipohutubia mkutano wa hadhara jijini Dar es Salaam, baada ya ziara yake ya kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na vurugu wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika nchini Oktoba 29, 2025.

Wakati huo huo, Mwigulu amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameagiza maadhimisho ya Siku ya Uhuru ya Desemba 9, mwaka huu kutofanyika, badala yake fedha zilizotengwa kwa ajili ya shughuli hiyo zitumike kugharimia ukarabati wa miundombinu ya umma iliyoharibiwa wakati wa vurugu hizo.
Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu huyo ameagiza Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) na wadau wote wanaohusika wakae na kutengeneza utaratibu wa mpito ili kurejesha huduma za usafiri huo ndani ya siku 10.
Huduma za usafiri wa mabasi hayo zilisitishwa baada ya vurugu za Uchaguzi Mkuu mwaka huu - zilizosababisha kuchomwa moto kwa vituo vya mabasi na kuharibiwa kwa mifumo ya mawasiliano na ukusanyaji nauli.
Sambamba na hilo la ukarabati wa miundombinu, Waziri Mkuu Mwigulu ameelekeza kuanzia sasa wakandarasi wazawa wapewe kipaumbele kwenye tenda za ujenzi wa miradi nchini.
"Wapatieni kazi wakandarasi wazawa, wana uwezo, hata kazi wanazopewa wageni, wakandarasi wazawa ndio wanafanya hizi kazi," amesema.
No comments:
Post a Comment