Kaimu Mkurugenzi wa TIA Kampasi
ya Tanga, Dkt Mwita Sospeter Mkami.
-------------------------------------
Na Mwandishi Wetu
Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) imetangaza kuanzisha tawi lake mkoani Tanga, hatua ambayo inahitimisha kiu ya muda mrefu ya mkoa huo ya kuwa na chuo cha elimu ya juu kinachotoa mafunzo ngazi ya shahada ya kwanza.
Hivyo, wananchi wa Tanga na mikoa jirani wana kila sababuya kufurahi kwa kupata fursa ya masomo kupitia Tawi la TIA Tanga lililosajiliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo Stadi (NACTVET).
Kozi zitakazotolewa katika tawi hilo ni pamoja na cheti cha awali, stashahada, shahada katika fani ya uhasibu, ununuzi na ugavi, na usimamizi wa rasilimali watu.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa TIA Kampasi ya Tanga, Dkt Mwita Sospeter Mkami, hatua ya kuanzisha tawi hilo ni sehemu ya mkakati wa makusudi wa kuunga juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, na utekelezaji wa Ilani ya chama tawala - CCM.
“Rais Samia amedhamiria kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya elimu, akitambua kwamba elimu ni chachu ya maendeleo ya taifa,” Dkt Mwita alisema katika mazungumzo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, wiki iliyopita.
Dkt Mwita aliongeza: “Jitihada hizi za kuanzisha Tawi la TIA Tanga ni muhimu kwa sababu zitawezesha wananchi wa Tanga na maeneo jirani kupata elimu bora karibu na nyumbani mwao. Hii ni fursa kubwa ya kujiendeleza kielimu na kuongeza maarifa katika fani mbalimbali.”
Kwa hivyo, wana-Tanga na wananchi wa mikoa jirani wanahamasishwa kuchangamkia fursa ya kuanzishwa kwa tawi hilo la TIA katika kupata elimu - kama hatua muhimu ya kujiletea maendeleo binafsi na kuimarisha uwezo wa kitaaluma.
No comments:
Post a Comment