
Mwenyekiti wa UWT CCM Taifa, Mary Chatanda.
-------------------------------------------
Na Mwandishi Maalumu
Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) CCM Mkoa wa Mara umeweka mipango maalumu itakayousaidia kujiimarisha kiuchumi na kuongeza ufanisi katika utendaji wake.
Tayari umoja huo umezindua harambee itakayouwezesha kupata mamilioni ya fedha kwa ajili ya kuanzisha miradi ya kiuchumi na kupunguza utegemezi.
Uzinduzi wa harambee hiyo ulifanyika kimkoa katika hoteli ya CMG wilayani Tarime wiki iliyopita.
Shilingi milioni 57 zilipatikana zikiwemo fedha taslimu milioni 37 katika uzinduzi huo ambao ulibebwa na kupambwa na makada wa chama hicho tawala, akiwemo Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Joyce Mang’o.
Mgeni rasmi katika harambee hiyo alikuwa Mjumbe wa NEC CCM Taifa, Hellen Boghohe ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda.
“Tunashukuru Mungu, katika uzinduzi tulipata shilingi milioni 57, kati ya hizo, cash (taslimu) ni shilingi milioni 37 na nyingine ni ahadi,” Mwenyekiti wa UWT CCM Mkoa wa Mara, Nancy Msafiri aliliambia Gazeti la Sauti ya Mara kwa njia ya simu juzi.
Nancy alisema shughuli nyingine kama hiyo inatarajiwa kufanyika baadaye ili kufikia malengo yao.
“Huu ulikuwa ni uzinduzi tu, fainali inakuja ambapo atakuja Mwenyekiti wa UWT Taifa mwenyewe, ndugu Mary Chatanda kupokea makusanyo yote,’ alifafanua.
Nancy alimwelezea Mwenyeti huyo wa UWT Taifa kama mtu mwenye upendo na maono ya kimaendeleo ambaye ameweka misingi mizuri katika ya kuijenga jumuiya hiyo CCM.
“Tunampenda sana Mwenyekiti wetu wa UWT Taifa [Mary Chatanda] kwani anatujali na kutuwekea mipango mizuri yenye tija kwa maendeleo ya UWT,” alisema Mwenyekiti huyo wa UWT CCM Mkoa wa Mara.
Alisema baadhi ya miradi ya kiuchumi wanayotarajia kuanzisha ni nyumba za kibiashara za kukodisha (maduka).
“Tunaenda kuanzisha miradi ya kiuchumi ili kuondokana na omba omba. Mfano, tuna vibanda ambavyo ni maboma, tunataka ujenzi wake ukamilike ili viwe sehemu ya mapato yetu kwa kuvipangisha.
“Tunataka kujiimarisha zaidi,” alisisitiza kiongozi huyo ambaye amewahi kuhudumu pia katika nafasi hiyo katika Serikali ya Awamu Nne chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete.
Aidha, Nancy alisema sehemu nyingine ya mapato itaelekezwa kwenye kuimarisha jumuiya kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Mbali na MNEC Joyce Mango, makada wengine wa CCM ambao wameonekana kupigia chapuo mipango hiyo ya kimaendeleo ndani ya jumuiya hiyo, ni Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Tarime, Neema Charles na Mjumbe wa Baraza Kuu la UWT Taifa, Rhobi Samwelly, kwa mujibu vyanzo vyetu kutoka ndani ya chama hicho.
“Pia Mwenyekiti wa CCM Mkoa, ndugu Chandi Marwa ni mtu wa maendeleo na baadhi ya wabunge kama vile Mheshimiwa Jafari Chege wa Rorya walichangia, ,’ alisema kada mmoja wa chama hicho kutoka jimbo la Musoma Mjini.
Makada wengine waliotajwa kuchanga fedha taslimu katika harambee hiyo ni aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime, Nyambari Nyangwine, Daniel Chonchorio, DC Juma Chikoka, DC Amina Makilagi, Kambarage Wasira na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Wilfred Nyihita.
UWT ni moja ya jumuiya za CCM zinazotajwa kuwa na nguvu kubwa ya wanawake, hasa unapofika wakati wa masuala ya uchaguzi ndani na nje ya chama hicho tawala.
No comments:
Post a Comment