
Waziri Simbachawene (mwenye suti nyeusi), Naibu Waziri Jumanne Sagini (mwenye miwani nyumba ya Simbachawene), Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (mwenye kofia) na viongozi wengine wa chama na serikali wakifurahia uzinduzi wa Shule ya Msingi Chief Manyori katika kijiji cha Nyamisisi wilayani Butiama jana.
-----------------------------------------
Butiama
Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utwala bora, George Simbachawene ameeleza kuridhishwa kwake na miradi ya maendeleo ya wananchi inayotekelezwa mkoani Mara.
Amesema hali hiyo inatokana na msukumo unaotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni sehemu ya kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarange Nyerere kwa vitendo.
"Hongereni kwa miradi mikubwa ya maendeleo, kuletwa fedha nyingi hapa ni maono na utashi wa Rais Samia. Mmepata miradi mikubwa ya elimu, afya, chuo kikuu, mradi wa maji Mgango-Kiabakari na mradi wa umeme wa Mwalimu Nyerere. Pongezi mlizotoa nitazifikisha kwa Rais," alisema Waziri Simbachawene.
Aliyasema hayo jana Oktoba 3, 2024 wakati wa uzinduzi wa shule mpya ya msingi ya Chief Manyori iliyojengwa katika kijiji cha Nyamisisi wilayani Butiama, Mara kwa gharama ya shilingi milioni 640 zilizotolewa na serikali.

Muonekano wa mbele wa jengo la utawala la Shule ya Msingi Chief Manyori katika kijiji cha Nyamisisi.
--------------------------------------------
Awali, akizungumza kwa niaba ya wananchi Mbunge wa Jimbo la Butiama, Jumanne Sagini alimshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi iliyokuwa imekwama kwa miaka mitatu, likiwemo jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.
"Tunaipongeza serikali kwa ilichowafanyia wananchi wa Nyamisisi kwa kujenga shule mpya ili kutoa fursa kila mtoto kupata elimu.
"Jengo la Halmashauri limekuja kukamilishwa na Dkt Samia, sekondari mpya nane, shule za msingi 12, kituo cha afya Kiagata, pamoja na ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia," alisema Sagini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi alimshukuru Rais Samia kwa kupeleka miradi kila sehemu nchini.
"Haijawahi kutokea mkoa wa Mara umepata trilioni moja na bilioni 220, kwa miradi 280 inayoendelea kutekelezwa, haitakaa itokee kupata Rais kama Samia, kila sehemu amegusa," alisema Mtambi.
Kiongozi huyo wa mkoa alitumia nafasi hiyo pia kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa viongozi serikali za mitaa watakaowaletea maendeleo.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>Katibu CCM Mara afungua kambi la mafunzo kwa vijana wa UVCCM, awataka kutokubali kutumiwa kuvuruga amani
>>Wanakijiji Serengeti 'wamwangukia' Waziri Simbachawene, aagiza wajengewe daraja
>>Tragedy on lake Kivu as ferry capsizes, claiming 78 lives
>>Hospitali ya Halmashauri Musoma Vijijini yaanza kuhudumia wananchi
No comments:
Post a Comment