NEWS

Monday, 20 January 2025

Nyambari ampongeza Wasira kuchaguliwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, asema ni kiongozi anayechukia rushwa



Stephen Wasira na Nyambari Nyangwine
 
 
Na Mwandishi Maalumu/ Mara Online News

Kada wa Chama Chama Mapinduzi (CCM), Nyambari Nyangwine amempongeza mwanasiasa maarufu nchini, Stephen Masato Wasira kwa kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, akimtaja kama kiongozi sahihi, jasiri, anayechukia rushwa na mwenye uwezo mkubwa wa kupangua hoja za wapinzani.

“Kwanza nampongeza mzee Wasira kwa ushindi mnono, ni jasiri na kiongozi anayechukia rushwa kwa vitendo,” Nyambari alisema jana katika mahojiano na Sauti ya Mara kwa njia ya simu kutoka jijini Dodoma.

Nyambari alimuelezea Wasira kama gwiji wa siasa za Tanzania ambaye ana uwezo mkubwa wa kujenga na kupangua hoja, zikiwemo za wapinzani.

“Wasira ni mtu anayejiamini na ana uwezo mkubwa wa kupangua hoja za wapinzani kwa mantiki,” alisema Nyambari ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime, mkoani Mara kwa tiketi ya CCM.

Aliendelea kummiminia Wasira sifa akisema ni mtu mtulivu, mnyenyekevu, mweye huruma na kongozi anayeijua historia ya Tanzania vizuri.

Aidha, Nyambari alisema Wasira amekuwa ‘role model’ na mwalimu wake katika siasa.

“Mzee Wasira ni ‘role model’ wangu katika siasa na mimi ni mwanafunzi wake kwenye siasa, nimeendelea kuvutiwa naye na kuvuna mambo mengi kwakwe,” aliongeza Nyambari ambaye ni mfanyabiashara, mchapishaji na mwandishi wa vitabu maarufu nchini.

Nyambari ambaye pia alihuduhuia kama mgeni mwalikwa katika Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Taifa uliomchagua Wasira jijini Dodoma juzi Jumamosi, alisema ushindi wa Wasira katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni faida kwa taifa la Tanzania.

“Wasira atakisadia chama chetu cha CCM sana na nchi yetu kwa ujumla,” alisema Nyambari ambaye anajipambanua pia kama kada mtiifu wa CCM.

Wasira alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tannzania Bara kwa kura za ndiyo 1,910 kati ya 1,921 zilizopigwa na wajumbe wa mkutano huo.

Kura za hapana ni saba na zilizoharibika ni nne katika uchaguzi huo.

Wasira amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Kanali Abdulrahman Omar Kinana ambaye alijiuzulu nafasi hiyo Julai 2024.

Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Taifa ulimalizika jana Jamapili, kwa kujadili utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 na taarifa za utendaji kwa serikali zote mbili (Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar).
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages