Na Mwandishi Wetu
Tanzania imeyahakikishia mataifa ya magharibi, ikiwemo Marekani, kwamba Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu utakuwa huru na wa haki.
Makamu Mwenyekiti wa chama tawala cha CCM upande wa Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema kwamba kwa kuwa taifa hili kubwa la Afrika Mashariki limo katika safari ya maendeleo haliwezi kuwekwa rehani kwa kudharau tunu ya amani.
Wasira aliyasema hayo mjini Dar es Salaam jana alipokuwa na mazungumzo na Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Andrew Lentz.
Alimwambia nwanadiplomasia huyo kuwa Chama Cha Mapinduzi kinaendelea kujiandaa kwa uchaguzi ujao na kwamba kinatarajia kuvuna ilichopanda kwa kupata ushindi kwa sababu kimekuwa mstari wa mbele katika kutekekeza kwa umakini Ilani yake ya mwaka 2020-2025.
Alisema CCM kwa ukongwe wake wakati wote ipo tayari kuzungumza na vyama vya upinzani ambao ni msingi wa falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kufikia maridhiano kwa masuala muhimu ya taifa.
Wakati huo huo, Wasira jana hiyo hiyo alifanya mazungumzo na Balozi wa Cuba nchini, Yordenis Despaigne.
Mazungumzo ya viongozi hao wawili yalijikita katika kuimarisha uhusiano uliopo baina ya nchi hizo mbili tangu enzi za viongozi waasisi wa Tanzania na Cuba, Mwalimu Julius Nyerere na mwananapinduzi Fidel Castro.
No comments:
Post a Comment