
Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi
Na Mwandishi Wetu
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi, ataanza ziara ya siku tano mkoani Mara kuanzia Jumanne wiki ijayo, kukagua shughuli mbalimbali za chama hicho tawala.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Idara ya Siasa, Uenezi na Mafunzo CCM Mkoa wa Mara leo, Dkt Nchimbi atatembelea wilaya za Bunda, Musoma, Butiama, Rorya, Tarime na Serengeti.
Hii itakuwa ni ziara ya kawaida kwa kiongozi huyo kujionea utekelezaji wa ahadi zilizotolewa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020-2025.
Mkoa wa Mara ndipo alikozaliwa gwiji wa siasa Tanzania na barani Afrika, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye aliendesha harakati za kuwang’oa wakoloni wa Kiingereza mwaka 1961.
Mkoa huo pia ndipo anakotoka Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira, ambaye tangu ujana wake amelitumikia taifa katika nyadhifa mbalimbali serikalini.
Kwa Dkt Nchimbi, hii itakuwa ni fursa yake nyingine kuutembelea mkoa wa Mara kama Makamu wa Rais mtarajiwa baada ya Mkutano Mkuu wa CCM kumteua mapema mwa huu kuwa mgombea mwenza wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu wa 2025.
No comments:
Post a Comment