NEWS

Saturday, 12 April 2025

Mabilioni ya fedha za mrabaha, CSR kutoka Mgodi wa Barrick North Mara yafungua zama za ustawi kijijini Genkuru



Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Genkuru, Juma Elias Kegoye, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) waliotembelea kijijini hiapo Aprili 11, 2025.
------------------------------------------

Na Christopher Gamaina, Tarime

Kijiji cha Genkuru kilichopo kata ya Nyarokoba katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, sasa kina kila sababu ya kuwa mfano bora wa ustawi wa kijamii na kiuchumi, kutokana na mavuno ya mabilioni ya fedha za mrabaha na Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) kinayopata kutoka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.

Genkuru ni miongoni mwa vijiji vitano vinavyopata malipo ya gawio la mrabaha kila robo ya mwaka kutoka kwenye mgodi huo. Vijiji vingine ni Nyangoto, Kerende, Nyamwaga na Kewanja.

Vijiji hivyo ni ambavyo vilikuwa na haki ya kuchimba dhahabu kwenye shimo la Nyabigena (ambalo ni sehemu ya mgodi wa North Mara) kabla ya kampuni ya Barrick kukabidhiwa kuendesha mgodi huo kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals kuanzia mwaka 2019.

Lori likiwa kazini katika Mgodi 
wa Dhahabu wa North Mara.

Kwa sasa kijiji cha Genkuru kinamiliki shilingi zaidi ya bilioni mbili za mrabaha, ambazo ni malipo ya robo nne za mwaka zilizotolewa na mgodi huo miezi michache iliyopita kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kijamii.

“Mpaka sasa hivi ninapozungumza nanyi, nina shilingi zaidi ya bilioni mbili kwenye akaunti ya kijiji,” Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Genkuru, Juma Elias Kegoye, aliwambia waandishi wa habari waliotembelea kijijini hapo juzi Ijumaa.

Fedha hizo zimewapa wanakijiji matumaini ya kuelekea kwenye zama za ustawi, kwani tayari zimepangiwa matumizi ya kugharimia ujenzi wa barabara mpya zisizo za lami ndani ya kijiji hicho, kwa mujibu wa Kegoye.

Mbali na gawio la mrabaha, kijiji hicho pia hupokea mgawo wa mamilioni mengine ya fedha yanayotolewa kila mwaka na kampuni ya Barrick kupitia mpango wake wa CSR.

Fedha za CSR nazo hutumika kugharimia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii kwa lengo la kuinua ustawi wa maisha ya wakazi wa kijiji cha Genkuru, miongoni mwa vijiji vingine.

Kwa sasa fedha za CSR zinatumika kugharimia ujenzi wa uzio wa bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari Bwirege, vyumba vitatu vya madarasa na matundu 16 ya vyoo vya wanafunzi katika shule ya msingi mpya Kurumwa.

“Sehemu nyingine ya fedha za CSR kwa sasa inatumia kugharimia ujenzi wa uzio wa Kituo cha Afya Genkuru na ukarabati wa barabara zilizopo ndani ya kijiji chetu,” aliongeza Kegoye.

Kituo cha Afya Genkuru kinahudumia kata ya Nyarokoba inayoundwa na vijiji viwili vya Genkuru na Msege vyenye wakazi zaidi ya 12,000, kwa mujibu wa Afisa Mtendaji wa Kata hiyo, Flora Maginga.

Sehenu ya majengo ya Kituo cha Afya Genkuru. (Picha zote na Mara Online News)

Kwa mujibu wa Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Francis Uhadi, shilingi zaidi ya bilioni tisa zimetolewa na mgodi huo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kijamii mwaka huu.

Asilimia 40 ya fedha hizo imeelekezwa kwenye vijiji 11 vilivyo jirani na mgodi huo, huku asilimia 60 ikipelekwa katika vijiji 77 vinavyosalia katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

“Lengo la mgodi ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma nzuri za kijamii,” alisema Uhadi.

Miradi yote ya kijamii inayoibuliwa na kupangwa na wanakijiji ni yenye lengo la kuboresha huduma muhimu kama vile afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara.

Kijiji cha Genkuru kwa sasa kina wakazi zaidi ya 5,600, kwa mujibu wa Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Waitara Kemo.

Wakazi wa Genkuru waliozungumza na Mara Online News walisema utekelezaji wa miradi ya kijamii kutokana na fedha za mrabaha na CSR, ni ushuhuda wa namna rasilimali za taifa, yakiwemo madini - zinavyoweza kuwa chachu ya maendeleo ya jamii, na hasa pale zinaposimamiwa kwa uwazi na uadilifu.

“Ni matarajio ya wengi kuwa rasilimali hizo zitaendelea kutumika kwa busara ili kuleta tija na ustawi wa kweli kwa wananchi wa kijiji cha Genkuru,” alisema mkazi wa kijiji hicho aliyejitambulisha kwa jina la Maria Matinde.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages