
Mhandisi Boniface Gissima Nyamo-Hanga enzi za uhai
Na Mwandishi Wetu, Bunda
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Taifa la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Boniface Gissima Nyamohanga na dereva wake, Muhajiri Mohamed Haule, wamefariki dunia katika ajali ya gari saa 7:00 usiku wa kuamkia leo Aprili 13, 2025 wilayani Bunda, mkoani Mara.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evansi Mtambi na Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Pius Lutumo, wamethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
Kamanda Lutumo amesema gari aina ya Toyota Land Cruiser walilokuwa wakisafiria kutokea mkoani Mwanza liligongana uso kwa uso na lori na kusababisha vifo vyao.
Inaeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa gari la Mhandisi Nyamohanga ambaye alijaribu kumkwepa mwendesha baiskeli hali iliyomsababisha kupoteza mwelekeo.
Miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda kusubiri taratibu nyingine.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi akieleza kusikitishwa mno na taarifa ya vifo vya watumishi hao wa umma.
“Ninatoa pole kwa familia, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt Doto Biteko, watumishi wa TANESCO, ndugu, jamaa na marafiki.
“Ninamuomba Mwenyezi Mungu azijaalie familia, ndugu, jamaa na marafiki subra, uvumilivu na moyo wa ibada katika kipindi hiki kigumu. Mwenyezi Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi. Amina,” Rais Samia ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii leo.
No comments:
Post a Comment