NEWS

Sunday, 19 October 2025

PMF Mara Qwan Ki Do International yaing’arisha Tanzania mashindano ya Africa Qwan Ki Do 2025


Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, akikabidhi cheti cha pongezi kwa mmoja wa wachezaji wa PMF Mara Qwan Ki Do International walioshinda medali ya dhahabu ya mashindano ya Africa Qwan Ki Do 2025.

Na Mwandishi Wetu
Tarime
-------------

Klabu ya Mchezo wa Mapigano ya PMF Mara Qwan Ki Do International iliyopo Tarime, imeiheshimisha Tanzania katika mashindano ya mchezo huo barani Afrika, baada ya kuvuna medali nane za dhahabu na kushika nafasi ya sita kati ya vilabu 14 vilivyoshiriki.

PMF Mara Qwan Ki Do International ni miongoni mwa vilabu vitatu vilivyoiwakilisha Tanzania katika Mashindano ya Tatu ya ‘Africa Qwan Ki Do Championships Online’, yaliyohusisha watoto na vijana wenye umri kati ya miaka saba na 17 kutoka nchi mbalimbali.

Wawakilishi wengine wa Tanzania ni vilabu vya Mwanza Kung Fu Tai Chi na Bamma Qwankido ambao walishiriki na kushika nafasi ya nne, hivyo kuiwezesha Tanzania kushika nafasi ya tatu kati ya nchi 16 zilizoshiriki.

Katika ushindi huo wa nafasi ya tatu, Tanzania ilitanguliwa na nchi za Morocco na Ivory Coast. Hivyo, kwa ushindi huo, Tanzania imechaguliwa kushiriki mashindano ya dunia ya Qwan Ki Do mwanzoni mwa mwaka 2026.

Nchi nyingine zilizoshiriki mashindano hayo yaliyofanyika Mei 17, 2025 ni pamoja na Senegal, Gabon, Bukina Faso, DRC Congo na Africa Kusini.

Kutokana na ushindi huo wa PMF Mara Qwan Ki Do International, wachezaji wake 16 wametunukiwa vyeti na medali kwa washindi wanane, wakiwemo wasichana watatu walioshinda dhahabu, ilikuwatia moyo na kuwapongeza kwa kupeperusha vizuri bendera ya Tanzania katika mashindano hayo ya kimataifa.


Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (aliyevaa skafu) na Mgombea Ubunge Jimbo la Tarime Mjini, Esther Matiko (CCM), wakikabidhi cheti cha pongezi kwa mmoja wa wachezaji wa PMF Mara Qwan Ki Do International alioshinda medali ya dhahabu ya mashindano ya Africa Qwan Ki Do 2025.


Baadhi ya wachezaji wa PMF Mara Qwan Ki Do International wakionesha ufundi wao.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, aliwakabidhi washiriki hao vyeti mbele ya Mkurugenzi wa Ufundi wa Qwan Ki DO Tanzania, Zachary Zolla, wakati wa Mahafali ya Nane ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Tarime Mchanganyiko, yaliyofanyika shuleni hapo Oktoba 17, 2025.

Aidha, mgombea katika jimbo la Tarime Mjini kupitia CCM, Esther Matiko, aliwakabidhi washindi wa kike nishani za dhahabu kwa heshima ya wanawake kwenye mchezo huo.

Meja Gowele aliipongeza Taasisi ya Professor Mwera (PMF) inayomiliki shule hiyo kwa kuanzisha mchezo wa Qwan Ki Do wilayani Tarime.

"Niipongeze PMF kwa namna mnavyojali michezo, hasa kwa kuleta mchezo huu hapa Tarime maana unahamasisha discipline (nidhamu), unafanya vijana waweze kujiamini, lakini pia kuwa tayari wakati wote hata katika masomo," alisema Gowele.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa PMF, Hezbon Peter Mwera, ambaye ni Mwalimu Mwanafunzi Msaidizi wa Qwan Ki Do alitunukiwa vazi maalum kutoka Ubelgiji kama Mwalimu Msaidizi wa mchezo huo, alisema ushindi walioupata umewaongezea ari ya kujiandaa ili kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya kidunia yajayo na kuiletea Tanzania medali nyingi zaidi.


Mkurugenzi wa Ufundi wa Qwan Ki DO Tanzania, Zachary Zolla (kushoto), akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa PMF, Hezbon Peter Mwera, vazi maalum la Qwan Ki Do kutoka Ubelgiji kutambua mchango wake kwa mchezo huo.

Awali, Zolla akizungumza kwa niaba ya Shirikisho la Dunia la Qwan Ki Do na Qwan Ki Do Tanzania, alisema mchezo huo ni sanaa ya mapigano wenye asili ya China na Vietnam iliyoanzishwa mwaka 1981 na kwamba uliingia Tanzania mwaka 2020, ambapo mpaka sasa nchi 36 duniani zinaushiriki.

Zolla ambaye pia alishinda Tuzo ya Mwamuzi Bora katika mashindano hayo, alisema Qwan Ki Do hufanyika kila mwaka kwa kila nchi na kila baada ya miaka miwili katika ngazi ya Afrika, ambapo washindi hushiriki mashindano ya dunia.

Mbali na Shule ya Sekondari Tarime Mchanganyiko, Taasisi ya PMF inamiliki pia Shule ya Msingi Mwera Vision, Jogging Club, Mwera Jazz Band, PMF Restaurant na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime kinachotoa mafunzo ya fani tofauti zikiwemo za ufundi magari, umeme, mabomba, uhazili, udereva, ushonaji, uongozaji watalii na upishi, miongoni mwa nyingine.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages