Na Mwandishi wa Mara Online News
Bilionea Mwingereza na mmiliki mwenza wa Klabu maarufu ya kandanda ya Manchester United, Sir Jim Ratcliffe, ameeleza dhamira yake ya kuitumia klabu hiyo kongwe barani Ulaya kukuza tasnia ya utalii nchini Tanzania.
Tajiri huyo alielezea nia hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati wa majadiliano yake na Rais Samia Suluhu, mazungumzo ambayo yalijikita kwenye uhifadhi, utalii na maendeleo ya michezo.
Taasisi ya Sir Jim Ratcliffe’s ya Six Rivers imefanya kazi kubwa ya kusaidia juhudi za uhifadhi kwa kushirikiana na Shirika la Uhifadhi Tanzania (TANAPA) na Taasisi ya Utafiti Wanyamapori (TAWIRI) katika kutafuta ufumbuzi wa migogoro ya ardhi kati ya binadamu na wanyamapori.
“Leo nimekuwa na mazunguzo na mmoja wa wamiliki wa Klabu ya Mpira wa Miguu ya Manchester United, Sir Jim Ratcliffe. Mazungumzo hayo yalilenga ushirikiano katika masuala ya uhifadhi na utafiti. Sir Ratcliffe ameeleza dhamira yake ya kuitumia Klabu ya Manchester United kutangaza utalii wa Tanzania,” Rais alisema baada ya mkutano wake na bilionea huyo.
“Nimesikiliza dhamira ya Sir Ratcliffe ya kuitumia Klabu ya Manchester United kutangaza utalii wa Tanzania na nimemkaribisha kuanzisha vituo vya michezo. Pia nimepokea jumbe mbalimbali zinazonitakia heri kutoka kwa Kocha Mkuu wa United, Ruben Amorim, kwa niaba ya wachezaji wa klabu hiyo na Kocha Mkuu wa zamani, Sir Alex Ferguson,” Rais Samia aliongeza.
Katika kipindi chake cha utawala wa miaka mine iliyopita, Rais Samia amejitahidi kutoa kipaumbele kwa maendeleo ya michezo ili Tanzania iweze kufikia hatua ya juu kama ilivyo kwa baadhi ya nchi nyingine duniani katika nyanja hiyo ambayo inawaunganisha watu wengi wa kila taifa bila kujali rangi.
Mkutano kati ya Rais Samia na mgeni wake Sir Jim Ratcliffe ulihudhuriwa pia na viongozi wa ngazi za juu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, akiwemo Waziri Pindi Chana, Katibu Mkuu, Hassan Abbas, Kamishina wa Uhifadhi wa TANAPA Juma Nassoro Kuji, pamoja na viongozi wa idara na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo.
Inatarajiwa kuwa ziara ya Sir Jim Ratcliffe itakuwa kichocheo cha kuwavuta watalii wengi nchini Uingiereza kuja Tanzania kuona vivutio vingi vya utalii kuanzia fukwe zilizofunikwa na minazi za Bahari ya Hindi hadi Mlima Kilimanjaro, ambao ni fahari ya Tanzania na Afrika.
No comments:
Post a Comment