NEWS

Friday, 9 May 2025

Mkuu wa Mkoa asisitiza mikakati ya kuongeza uzalishaji mazao ya kilimo akifungua Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Ushirika Mara



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi
(aliyevaa miwani waliokaa) na viongozi wengine mbalimbali katika picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya Jukwaa la Ushirika la mkoa huo wakati wa mkutano mkuu wao mjini Musoma jana.
------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Musoma

Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi, jana alifungua Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Ushirika la mkoa huo - uliofanyika mjini Musoma, na kusisitiza kuwepo na mipango madhubuti ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo ya kimkakati.

Alisema hatua hiyo itawezesha kukuza uchumi wa wakulima na kuongezeka mapato ya ushirika mkoani Mara.

"Ninakutakeni viongozi na watendaji kushirikiana na wataalamu wa ugani kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo ya kimkakati, ikiwemo kahawa, pamba, tumbaku na alizeti,” alisema Kanali Mtambi na kuzitaka mamlaka husika kuimarisha udhibiti wa vitendo vya utoroshwaji wa mazao kwenda nje ya nchi.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (kulia), akihutubia mkutano huo.
---------------------------------

Pia, Kanali Mtambi aliwahimiza wataalamu wa kilimo na ushirika kuimarisha mfumo wa stakabadhi ghalani ambao umeonesha matokeo chanya mkoani Mara, hasa kwenye zao la choroko.

Kiongozi huyo wa mkoa alisema kwamba mwanzoni zao hilo liliuzwa kwa shilingi 700 hadi 1,000 kwa kilo moja, lakini baada ya mfumo wa stakabadhi ghalani kutekelezwa bei imeongezeka kutoka shilingi 1,300 hadi 1,410 kwa kilo moja.

Awali, akisoma taarifa ya hali ya ushirika huo, Mrajis Msaidizi Mkoa wa Mara, Lucas Kiondele, alisema hadi sasa kuna vyama vya ushirika 308 na wakulima 11,665 katika mkoa huo.


"Kutekeleza mafanikio ya stakabadhi ghalani kwenye ushirika na wakulima kulipwa kwa njia za kidijitali (benki na simu), kusambaza mbolea za ruzuku kilo milioni zaidi ya milioni moja kwa wakulima mkoani Mara.

"Vyama vimetekeleza shughuli zake kupitia mfumo wa 'MUVU', taarifa zinawasilishwa kwa njia ya mtandao, hali iliyopunguza gharama na kuongeza ufanisi pamoja na vyama kujiendesha vyenyewe kupitia mitaji yao ya ndani, kutoa mikopo nafuu kwa wakulima, ajira za kudumu 346 na ajira za mikataba 119," alisema Kiondele.

Wadau waliohudhuria mkutano huo ni Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara (WAMACU Ltd), wakulima, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, watendaji wa serikali, wawakilishi wa COASCO na MOCU.
 (Picha zote na Mara Online News)
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages