
Mwenyekiti Momanyi Range (kushoto) akifurahia picha ya pamoja na wajumbe wake wa Kamati mpya ya Jukwaa la Ushirika Mkoa wa Mara wakati wa Mkutano Mkuu wa jukwaa hilo mjini Musoma jana Ijumaa.
--------------------------------------
Na Godfrey Marwa, Musoma
Wanaushirika mkoani Mara wamehimizwa kuchangamkia fursa ya Benki ya Ushirika Tanzania, ikiwa ni pamoja na kufungua akaunti na kupata mikopo nafuu ya mitaji kwa ajili ya kujiendeleza katika shughuli zao.
Rai hiyo ilitolewa na Mrajis Msaidizi (Uhamasishi na Uratibu) wa Tume ya Ushirika, Ibrahim Kadudu, katika hotuba yake ya kufunga Mkutano Mkuu wa siku mbili wa Jukwaa la Ushirika Mkoa wa Mara mjini Musoma jana Ijumaa.
"Tunayo Benki ya Ushirika, jitahidi mkafungue akaunti, Rais Samia katuchangia bilioni 10 [shilingi] za mtaji, anataka aone ushirika ulio imara na wenye kutoa matokeo chanya kwa wakulima na kwa wanaushirika," alisema Kadudu.
Benki hiyo ilizinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan jijini Dodoma Aprili 28, 2025 kwa lengo la kutoa mikopo ya mitaji nafuu ili kuwashirikisha wananchi wengi zaidi kupitia ushirika na kilimo katika kutoa mchango wao kwa uchumi wa taifa.

Mrajis Msaidizi, Ibrahim Kadudu, akizungumza katika mkutano huo.
-----------------------------------
Aidha, Kadudu aliwapongeza wanachama wa Jukwa la Ushirika Mkoa wa Mara kwa kufanikisha mkutano huo ambao pia ulichagua kamati mpya ya jukwaa hilo.
"Mmefanya uchaguzi wa kidemokrasia, kila mmoja ameona thamani ya kura yake, hongera wajumbe mliochaguliwa," alisema.
Momanyi Range alifanikiwa kutetea nafasi ya Mwenyekiti wa kamati hiyo baada ya kupata kura zote za wajumbe. "Nawashukuru kwa kuniamini ili muendelee kunituma, mmeweza kutambua kazi nzuri iliyofanyika, mimi ni mtekelezaji," alisema.

Sehemu ya wajumbe mkutanoni.
---------------------------------------
Wadau waliohudhuria mkutano huo ni kutoka Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara (WAMACU Ltd), wakulima, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, watendaji wa serikali, wawakilishi wa COASCO na MOCU, miongoni mwa wadau wengine.
No comments:
Post a Comment