
Grace Kiwelu
Na Mwandishi Wetu
Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA) Mkoa wa Kilimanjaro, Grace Kiwelu, naye ametangaza kujivua uanachama wa chama hicho cha upinzani nchini.
Kiwelu ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Mwenyekiti Kamati ya Fedha wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini na Mjumbe wa Kamati Tendaji ya BAWACHA Taifa, alitangaza uamuzi wake huo katika mkutano na waandishi wa habari jana.
“Nilijiunga na chama hiki tangu mwaka 1992 nikiwa binti na leo nazeeka ndani ya chama, lakini leo nimesimama mbele yenu kwa maumivu makubwa kwa sababu nitasema mwishoni ninaenda wapi.
“Uamuzi ninaouchukua leo mnisamehe nakipenda, na niliipenda sana CHADEMA kwa sababu ilinipa heshima sana, kufika hapa nilipofika nilijengwa na CHADEMA lakini sasa itoshe kusema kuanzia leo tarehe 11 Mei, 2025 ninajiondoa rasmi Chadema, ninakwenda nyumbani.
“Bado nina nguvu, sisemi ninaacha siasa lakini acha kwanza nikapumzike, na ninamshukuru Mungu sana kwamba Aprili 27, mwaka huu Mungu alinipa mjukuu, nakwenda kulea mjukuu wangu. Nimechoka na matusi ya mitandaoni kila siku,” alisema Kiwelu ambaye pia amewahi kuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia CHADEMA.
“Chama changu nilikipenda sana na nilikitumikia kwa moyo wa dhati, tulizunguka nchi nzima hii kuijenga CHADEMA, tulikuwa tunazunguka na Mbowe kuhakikisha chama chetu kinaenea Tanzania nzima. Tulifanya ziara wakati huo tukiwa wabunge watano tu, mimi nikiwa mbunge mwanamke pekee.
“Tunazunguka na hatuna mwanachama hata mmoja huko tunapoenda. Tukifika tunashusha viti, tunafunga spika, tunahutubia miti na watoto. Leo namshukuru Mungu tumefika hapa.
“Lakini badala ya kuvuna heshima, tunavuna matusi. Tulishauri chama kwa nia njema kwamba tunahitaji ‘reforms’ ndio, lakini tusizuie uchaguzi. Unawezaje kuzuia uchaguzi wakati wewe siyo mshirika wa uchaguzi? Tunafanyaje mikutano wakati tumeshasema tunaenda kuzuia uchaguzi? Tunauzuiaje uchaguzi? Wakasema tutazuia kwa maandamano.
“Leo wananchi wangu wa Vunjo niwambie tunaandamana kuzuia uchaguzi, tunaanzia wapi tunaishia wapi? Wazee wangu wa Vunjo na vijana, tunaanzia wapi? Maandamano tunayofanya ama vijana wanaoandika leo kutukana baba na mama zao kwenye mitandao hutowaona kwenye maandamano.
“Leo Viongozi wanaona matusi hawakemei, kosa ni kumuunga mkono Mbowe na nilimuunga mkono kwa sababu ya mageuzi makubwa aliyoyafanya ndani na nje ya chama chetu. Bila Mbowe tusingekuwa na ChADEMA hii ya leo.
“Mbowe ana haki ya kupongezwa, kwa hiyo mimi nimechukua maamuzi tayari kwamba leo ninafikia mwisho wa kuwa mwanachama wa CHADEMA, niwashukuru Viongozi wangu wa BAWACHA kwa kuniunga mkono na tutakwenda pamoja kuendeleza mapambano ya haki za wanawake na wananchi wetu, kuyafikia malengo tuliyokuwa tumetegemea kuyafikia,” alihitimisha Grace Kiwelu.
No comments:
Post a Comment