
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde (katikati), akifurahia picha ya pamoja na baadhi ya vijana kutoka vijiji vinavyozunguka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara - waliokabidhiwa leseni za uchimbaji madini katika hafla iliyofanyika Nyamongo wilayani Tarime jana Mei 3, 2025.
------------------------------------
Na Mwandishi Wetu, Nyamongo
Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara imekabidhi leseni za uchimbaji madini kwa vikundi 48 vya vijana wapatao 1,736 kutoka vijiji mbalimbali vilivyo jirani na mgodi huo.
Mgodi huo uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara, unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga.
Akikabidhi leseni hizo kwa viongozi wa vikundi hivyo katika hafla iliyofanyika Nyamongo jana Mei 3, 2025, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alisema utekelezaji wa mradi huo wa leseni za uchimbaji kwa vijana ni maelekezo mahsusi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tannzania, Dkt Samia Suluhu Hassan.
Waziri Mavunde aliongeza kuwa mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Mining for Brighter Tomorrow (MBT), akisisitiza kuwa lazima uwe na mafanikio yaliokusudiwa.
Waziri Mavunde alisema leseni hizo zitawezesha vijana hao kupata ajira ya uhakika na kushiriki kikamilifu kwenye uchumi wa madini nchini.
“Huu ni mradi mkubwa wa kwana na wa kihistoria nchini. Seikali itaendelea kutoa leseni za uchimbaji lwa ajili ya vijana ya vijana kupata ajiraza kujipatia kipato ili kuboresha maisha yao,” alisema Waziri Mavunde.
Aliishukuru Kampuni ya Barrick kwa ushirikiano iliotoa katika kufanikisha mradi huo wa leseni za uchimbaji unaotarahiwa kunufaisha vijana kiuchumi na kuboresha maisha yao kupitia maeneo yaliyotengwa katika wilaya za Tarime, Serengeti na Butiama mkoani Mara.
“Napenda kuipongeza Barrick North Mara kwa hatua hii nzuri. Tulizungumza tukaelewana kwa urahisi sana,” Waziri Mavunde alisema huku akiuita mradi huo kuwa wa kihistoria nchini Tanzania na wenye lengo la kuleta manufaa makubwa ya kiuchumi kwa vijana.
Hivyo, alimshukuru Meneja wa Barrick Tanzania, Dkt Melkiory Ngido na wasaidizi wake wote kwa ushirikiano mkubwa walioutoa.
Aidha, alidokeza kuwa tayari wadau kadhaa wakiwemo Benki ya Dunia, Baraza la Dhahabu Duniani na Benki ya Azania Tanzania wameonesha nia ya kushirikiana na serikali katika kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa manufaa.
“Benki ya Dunia, imevutiwa sana na mradi huu, vijana twendeni tukafanye kazi,” alisema Waziri huyo wa Madini.

Sehemu ya vijana wachimbaji wadogo wa madini wakifuatilia hotuba ya Waziri Mavunde katika hafla hiyo.
-----------------------------------
Waziri Mavunde aliwataka vijana hao kutumia fursa hiyo adhimu vizuri, huku akiwaahidi kuwa serikali itakuwa nao bega kwa bega kuhakikisha kuwa mradi huo wanawatoa kimaisha.
Aidha, alitangaza kuwa walezi wa mradi huo wa vijana wachimbaji watakuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, Meneja wa Barrick nchini Tanzania, Melkiory Ngido na yeye [Waziri Mavunde].
Awali, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko, aliipongeza Seikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia kwa kufanikisha hatua hiyo ya mradi wa vijana wachimbaji madini, akisema umefungua zama mpya kwa vijana ambao hawakuwa na ajira ya kujipatia kipato kwa ustawi wa maisha yao na familia zao.
Vijana wanaokwenda kunufaika na mradi huo waliishukuru Serikali ya Awamu Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia leseni hizo.
“Uchimbaji wa madini una faida, tuna matarajio ya kuinua kipato chetu, tumefurahi sana na tunamshukuru Mheshimiwa Rais wetu,” Deborah Daniel Ryoba kutoka kikundi cha Nyabikondo Mining.
Uzinduzi wa mradi huo ulishuhudiwa pia na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Flowin Gowele na Meneja Mahusiano wa Mgodi wa North Mara Francis Uhadi.
Wengine ni madiwani, watendaji wa kata na vijiji na wenyeviti wa serikali za vijiji vilivyo jirani na mgodi wa North Mara, miongoni mwa wageni waalikwa na wananchi wengine.

Katika hatua nyingine, Mgodi wa Dhahabu wa North Mara ulitumia fursa hiyo pia kukabidhi hundi zenye thamani ya shilingi bilioni 1.498 za mrabaha kwa vijiji vitano vilivyo jirani na mgodi huo ikiwa ni malipo ya robo ya kwanza kwa mwaka 2025.Vijiji hivyo ni Nyangoto, Kerende, Nyamwaga, Genkuru na Kewanja.
No comments:
Post a Comment