
Na Mwandishi Wetu/ Mara Online News
Kwa mara nyingine, Mbunge wa Butiama mkoani Mara, Jumanne Sagini, ametoa ng’ombe 500 kuchinjwa na kugawanywa kwenye vitongoji 370 na taasisi zote za umma na binafsi zilizopo katika jimbo hilo, kwa ajili ya kitoweo kwa wananchi kipindi hiki cha kusherehekea Sikukuu ya Eid Al-Adha.
Ugawaji wa sadaka hiyo adhimu umefanyika kwa siku mbili mfululizo - jana na leo, ikiwa ni sehemu ya kuonesha moyo wa upendo, ukarimu na mshikamano wa Mbunge Sagini kwa wananchi wa jimbo hilo.

Mbunge wa Jimbo la Butiama,
Jumanne Sagini.

Miongoni mwa taasisi zilizopata mgao huo wa ng’ombe ni misikiti na makanisa mbalimbali, familia ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Chifu Ihunyo, Chifu Wanzagi na Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT).
“Ni nadra sana kuona kiongozi mwenye moyo wa kujitolea kwa kiwango hiki. Tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu azidi kumpa afya na baraka,” mmoja wa wakazi wa Butiama amesema.
Kwa mujibu wa Afisa Habari wa Ofisi ya Mbunge Jimbo la Butiama, James Timba, hiyo ni mara ya pili kwa Mbunge Sagini kutoa sadaka ya ng’ombe kwa ajili ya kitoweo kwa wananchi wa jimbo hilo, ambapo mara ya kwanza alifanya hivyo mwaka 2022.
Hatua hiyo ya Mbunge Sagini inatajwa kuendelea kuimarisha upendo na mshikamano wa wana-Butiama, bila kujali tofauti za imani za kidini, kabila na itikadi za kisiasa.
No comments:
Post a Comment