
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde (aliyevaa shati jeusi) na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, wakiteta jambo kwa furaha wakati wa matembezi maalum kabla ya kuhitimisha Kongamano na Maonesho ya Madini Mkoa wa Mara 2025 mjini Musoma wiki iliyopita.
--------------------------------------------
NA MWANDISHI WETU, Musoma
MKOA wa Mara kupitia kwa wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa umezalisha dhahabu tani 58.9 yenye thamani ya shilingi trilioni 6.9 katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Afisa Madini Mkazi, Mhandisi Amini Msuya, alitoa taarifa hiyo wakati wa uhitimishaji wa Kongamano na Maonesho ya Madini Mkoa wa Mara 2025 mjini Musoma wiki iliyopita.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa huo, Kanali Evans Mtambi, alisema sekta ya madini inachangia asilimia 18 ya pato la mkoa huo wenye utajiri mkubwa wa madini Kanda ya Ziwa.
Mgeni rasmi, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, yeye alitaja mafanikio 16 yaliyopatikana kwenye sekta ya madini ndani ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia.
Pamoja na mafanikio mengine, Waziri Mavunde alisema maelekezo ya Rais Samia yamewezesha upatikanaji wa fedha nyingi kutoka serikalini kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya sekta ya madini nchini.
Alisema bajeti ya Wizara ya Madini imepanda kutoka shilingi bilioni 89 hadi 224, lakini pia mchango wa sekta ya madini kwa pato la taifa umeongezeka kutoka asilimia 7.2 hadi 10.1 kufikia mwaka jana.
Waziri Mavunde alitaja mafanikio mengine kuwa ni ujenzi wa masoko 43 na vituo zaidi ya 100 vya dhahabu pamoja na maabara kubwa ya kisasa kwa ajili ya kupima sapuli za madini kwa gharama nafuu.
“Pia, makusanyo ya madhuhuri yanayoingia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali yameongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 755 mwaka jana, huku asilimia 40 ya fedha hizo ikichangiwa na wachimbaji wadogo,” alisema.

Waziri Mavunde, akionesha Tuzo ya Pongezi iliyotolewa na Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini Mkoa wa Mara kumtunuku Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutambua mchango wake katika kukuza sekta ya madini na kuwainua wachimbaji wadogo Tanzania.
-------------------------------------------
Kuhusu akiba ya dhahabu ya kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Waziri Mavunde alisema wamenunua tani 3.7 katika kipindi cha miezi minane iliyopita na hivyo kuiwezesha Tanzania kuingia kwenye orodha ya nchi 10 bora barani Afrika.
Aidha, mwaka jana serikali kupitia Wizara ya Madini ilifuta leseni na maombi 2,648 ya uchimbaji madini kwenye maeneo yaliyokuwa wanashililiwa bila uchimbaji, kisha kuyagawa kwa wachimbaji wadogo.
Zaidi ya hayo, hivi karibuni, Waziri Mavunde aligawa leseni za uchimbaji madini kwa vikundi 48 vya vijana vyenye wanachama zaidi ya 2,000 mkoani Mara kwa ajili ya kuanza uchimbaji kwenye maeneo mbalimbali, yakiwemo yaliyokuwa yanamilikiwa na kampuni ya Barrick na serikali.
“Mwezi ujao vijana hawa wataanza rasmi uchimbaji baada ya kupata mafunzo maalum chini ya mradi mkubwa wa kuwezesha vijana, na tayari Benki ya Dunia (WB) na Baraza la Dhahabu la Dunia wamekubali kusaidia mradi huu ambao utagusa maeneo mengine,” waziri huyo alisema.
Kwa upande mwingine, alisema Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limetekeleza maelekezo ya Rais Samia ya kununua mitambo 15 ya kuchoronga miamba, ambapo mitano imeshasambazwa nchini na 10 inaingia siku chache zijazo kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini wanawake na vijana.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA), John Wambura Bina, aliwataka vijana kujipanga kumiliki uchumi wa madini na kuachana na migogoro.
No comments:
Post a Comment