NEWS

Sunday, 3 August 2025

Butiama: Jumuiya ya Tuko Sawa yazindua ‘Kizazi Cha Harmony’ nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere



Washiriki wa hafla ya uzinduzi wa ‘Kizazi Cha Harmony’ iliyoandaliwa na Jumuiya ya Tuko Sawa wakifurahia picha ya pamoja nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere – Mwitongo, Butiama mkoani Mara juzi.
-------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Butiama

Mlezi wa Jumuiya ya Tuko Sawa (JTS), Godfrey Madaraka Nyerere, amepokea rasmi Tuzo ya Profesa wa Harmony kwa niaba ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ikiwa ni kutambua mchango wake usiofutika katika kusimika maadili ya utu, mshikamano na heshima kwa viumbe wote.

Madaraka ambaye ni mtoto wa Mwalimu Nyerere, alikabidhiwa tuzo hiyo wakati JTS ikizindua ‘Kizazi Cha Harmony’ katika hafla iliyofanyika Ijumaa iliyopita nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere - Mwitongo, wilayani Butiama, Mara.

Uzinduzi huo wa Kizazi Cha Harmony ulitajwa kuwa ni sehemu kuu ya maono ya JTS ya kuifanya Tanzania kuwa kinara wa kimataifa katika harakati za kurejesha usawa wa asili (harmony), kuimarisha mshikamano na ushirikiano wa furaha.


Mlezi wa Jumuiya ya Tuko Sawa, Godfrey Madaraka Nyerere (katikati), akipokea Tuzo ya Profesa wa Harmony kwa niaba ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
------------------------------------------

JTS inatamani kuamsha mioyo ya mataifa mengine, hususan yale ya Jumuiya ya Madola – ambayo bado yanaheshimu hekima za Mababu, ili kushikamana kwa kutumia maarifa hai ya asili na hekima za kitamaduni kama zana kuu za kuponya dunia yetu inayoyumba.

“Sisi Wanaharmony tunaamini kabisa katika maneno ya kinabii ya Mfalme Charles III wa Uingereza, yaliyoandikwa kwenye kitabu chake cha Harmony, kwamba "siku itafika ambapo hekima ya Mababu itahitajika kutuokoa sisi pamoja na mazingira yetu – kwani teknolojia peke yake haiwezi kuwa jibu,” ilieleza taarifa ya JTS.

“Na sasa, kama jumuiya ya maadili ya ubinadamu, tunaweza kusema kwa sauti moja bila kupepesa macho: "Siku hiyo imefika - ni leo!" Tunapaswa kufanya marekebisho ya haraka, kwa moyo mmoja, ili kukabiliana na majanga makubwa yanayoikumba dunia ya sasa.

“Ndoto yetu ni dunia ambamo teknolojia na mila zinatembea bega kwa bega — kwa heshima, kwa usawa — zikiwainua wanadamu kutoka kwenye machafuko ya sasa na kuwaongoza kurudi kwenye mahusiano ya usawa kati ya viumbe wote na mazingira yao.

“Tunaiota Tanzania si tu kama “kisiwa cha utulivu”, bali kama wanaonesha njia wa maelewano ya kimataifa — mahali ambapo maadili ya ubinadamu, uzuri wa mazingira na ushirikiano wa furaha hukutana kwa ajili ya ustawi wa wote.

“Tunaona wageni kutoka kila pembe ya dunia wakiitembelea Tanzania, si kwa ajili ya mbuga au picha za wanyama tu — bali pia kwa ajili ya kuonja roho halisi ya Tanzania: kuketi nasi vijijini, kusikiliza hadithi zetu, kushiriki vyakula vyetu vya asili, na kuondoka wakiwa wamebeba si tu kumbukumbu, bali pia ufahamu mpya wa maana ya kuwa binadamu,” iliongeza taarifa ya JTS.


Mratibu wa Jumuia ya Tuko Sawa kutoka Arusha, Anna Kombe, akikabidhi mche wa mti wa matunda kwa Mlezi wa Jumuia hiyo, Godgrey Madaraka Nyerere (katikati) na Chifu wa Wazanaki, Japhet Wanzagi Nyerere wakati wa hafla hiyo.
-----------------------------------------

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa Chifu wa Wazanaki, Japhet Wanzagi Nyerere, ambaye alisisitiza umuhimu wa kuendelea kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.

"Ili tumuenzi mwalimu kwa dhati ni vizuri tukatembea katika misingi ile aliyoiasisi - misingi ya utu, umoja na upendo - kwamba utu wa mtu uthaminiwe apate haki zote kama mwanadamu bila ubaguzi wa rangi, dini, ukabila wala kikanda.

"Umoja wetu ndio ngao yetu kubwa, ndio msingi wa taifa letu, tuendelee kupandana na kujaliana," alisisitiza Chifu Wanzagi.

Kuhusu uhifadhi wa mazingira, Chifu Wanzagi alisema "Kwa kiasi tumepoteza miti ya asili ambayo ndiyo uumbaji wa Mungu, alivyoiumba hakuiacha aliiwekea miche mbalimbali ambayo ni uoto wa asili unaotuletea mvua, pia tunachimba dawa ambazo ni muhimu kwa binadamu."

Kwa upande wake, Mlezi wa JTS, Madaraka Nyerere, alisema jumuiya hiyo imebeba baadhi ya mambo ambayo Baba wa Taifa aliyasimamia.

“Mnaona kuna msisitizo kuwa wote Tuko Sawa, na sisi sote ni binadamu, hilo lilinivutia sana nilipoombwa kujiunga na jumuia hii,” alisema Madaraka.

Naye Mratibu wa Klabu za Jumuia ya Tuko Sawa, Conrad John Kiondo, alisema kupitia huu uzinduzi huo wa Kizazi Cha Harmony watapatikana vijana wanaojitambua. “Mahali popote penye upendo na umoja kuna maendeleo," alisema.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa pia na mabalozi wa JTS kutoka mikoa mbalimbali nchini, wanafunzi, viongozi wa serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Butima na wananchi wenyeji.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages